Katika kuelekea sikukuu ya Eid El Fitri, Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limefanya matendo ya huruma kwa kutembelea vituo viwili vya watoto wenye uhitaji na kutoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo mavazi, vyakula, pamoja na vifaa vya usafi.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo leo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani humo, Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Zauda Mohamed amesema wameona ni vyema kusherehekea sikukuu hiyo kwa kutembelea vituo hivyo vya watoto wenye uhitaji ambavyo ni Ummu Aisha na Kindness Children Care katika kuonesha upendo kwao.

Aidha, ACP Zauda ametoa wito kwa watu wengine wakiwemo watu binafsi, taasisi na vikundi mbalimbali kuwa na utaratibu wakuwatembelea watu wenye uhitaji katika jamii ili kutimiza malengo yao.

Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Ummu Aisha, Bw. Ally Shemkande amesema ujio wa Jeshi la Polisi katika kituo hicho si tu umeleta chakula mezani, bali umeleta matumaini na kuthaminiwa kwa watoto hao, ambapo ushirikiano huo unaimarisha dhana nzima ya ulinzi na usalama kwa jamii.Naye mkuu wa kituo cha Kindness Chilren Care, Bw. Yohana Mwampamba pamoja na kulishukuru Jeshi la Polisi kwa msaada wa vitu mbalimbali amewaomba wasichoke kwenda kuyatembelea makundi mengine yenye uhitaji katika jamii.

Nao baadhi ya watoto wamelishukuru na kulipongeza Jeshi la Polisi, kwa msaada wa vitu hivyo walivyopewa huku wakiwaomba wasichoke kuwatembelea mara kwa mara pindi wanapopata nafasi.