Naibu Waziri wa Maji, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bariadi MJINI *Mhe.Mhandisi Kundo Andrea Mathew,* amefanya ziara katika msikiti wa Mkoa wa Simiyu uliopo Jimbo la Bariadi Mjini kwa ajili ya kutoa mkono wa Idd kwa waamini wa dini hiyo wasio na uwezo ili washerekee vizuri sikukuu ya Idd.

 *Msaada huo ulijumuisha mchele kilo 300, sukari kilo 400, na tende kilo 100.*

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Mhandisi Kundo alisisitiza umuhimu wa kushirikiana na taasisi za dini katika kutoa msaada kwa wananchi na kuhakikisha kwamba familia maskini na wenye uhitaji wanapata msaada husika wakati wa sikukuu. 

Aliongeza kuwa ni wajibu wa viongozi kuhakikisha maendeleo ya jamii yanashirikisha sekta zote, ikiwemo elimu, huduma za kijamii, na misaada ya kibinadamu.

Kwa upande wake, Shekhe wa Mkoa wa Simiyu, *Issa Kwezi,* alimshukuru Mhandisi Kundo kwa moyo wake wa kujitolea na msaada wa mara kwa mara kwa taasisi za dini.

 Alibainisha kuwa Mhandisi Kundo amekuwa mchangiaji mkubwa katika maendeleo ya msikiti na shule ya Bariadi Islamic, kuanzia hatua za awali za ujenzi hadi sasa, jambo linalothibitisha ushirikiano wa dhati kati ya viongozi na jamii.

Msaada huu unalenga kutoa faraja na kuwaunga mkono wananchi wakati wa sikukuu ya Idd, sambamba na kuimarisha mshikamano wa kijamii na maendeleo endelevu katika Mkoa wa Simiyu.