
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mbunge wa Jimbo la Segerea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Mhe. Agnesta Kaiza, ametembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali muhimu katika Shule ya Msingi Buguruni Viziwi, jijini Dar es Salaam.
Msaada uliotolewa na mbunge huyo unajumuisha mahitaji ya kila siku, ikiwemo mchele, unga wa sembe, unga wa ngano, mafuta ya kupikia, sabuni za unga na za miche, miswaki, dawa ya meno, madaftari, kalamu, juisi, chumvi, sukari, maharage pamoja na vifaa vya kujifunzia.
Msaada huo umetolewa kama sehemu ya kuwafariji na kuwapa mkono wa heri watoto hao kuelekea sikukuu za Iddi na Pasaka.
Akizungumza Machi 17, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhi msaada huo kwa uongozi wa Shule ya Msingi Buguruni Viziwi, Mhe. Kaiza amesema kuwa watoto wenye uhitaji maalum wanahitaji uangalizi wa karibu ili waweze kufikia ndoto zao na kuishi katika mazingira rafiki.
Aidha, Mhe. Kaiza amesema kuwa katika shule hiyo kuna watoto 260, ambapo miongoni mwa changamoto zilizopo ni ukosefu wa mabweni ya kutosha, na hata lile lililopo ni la zamani ambalo haliendani na mahitaji ya sasa.
Mhe. Kaiza amesisitiza umuhimu wa jamii kwa ujumla kuwa na moyo wa kujali na kusaidia watoto wenye uhitaji, hasa makundi yenye mahitaji maalum, ili waweze kusoma katika mazingira rafiki.
Amesema ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha watoto hao wanapata fursa sawa za maisha, elimu na maendeleo ili waweze kufikia ndoto na malengo yao ya baadaye.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Buguruni Viziwi, Bw. Richard Kweka, amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Segerea kwa msaada huo mkubwa alioutoa, akieleza kuwa utasaidia kupunguza changamoto za mahitaji ya msingi kwa watoto katika shule hiyo.
Pia ametoa wito kwa jamii kuendelea kuwasaidia watoto wenye uhitaji ili waweze kupata elimu bora.
