NA DENIS MLOWE, IRINGA
STEVE Marwa, Meneja Mkuu wa Mradi wa Kilimanjaro Center for Community Ophthalmology (KCCO) mkoa wa Iringa amesema kuwa shirika hilo limekuwa likitekeleza mpango wa kutoa huduma za macho katika  mkoa wa  Iringa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na litandelea kwa kipindi cha angalau miaka mitatu.

Amesema lengo kuu ni kuwafikia wananchi wote wenye matatizo ya macho, hususan wale wanaohitaji upasuaji wa mtoto wa jicho na zoezi hilo limeandelea katika kituo cha afya cha Ipogoro mamia ya wakazi wamejitokeza kupata matibab ya macho..

Marwa amesema mpango huu unatekelezwa katika wilaya zote za mkoa wa Iringa, akizitaja kuwa ni pamoja na  Kilolo,  Mafinga,  Mufindi na maeneo mbalimbali ya  Iringa DC. Tangu kuanza kwa kampeni hiyo mwezi Oktoba mwaka jana, wananchi wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupata huduma hizo, ambazo zinatolewa bila malipo kwa uchunguzi na ushauri wa kitaalamu.

Wananchi huchangia gharama ndogo kwa vifaa kama miwani inapohitajika.

Amefafanua kuwa kila kata inatarajiwa kutoa kati ya watu 150 hadi 200 wanaopimwa macho, huku wale wanaohitaji upasuaji wa mtoto wa jicho wakifikishwa hospitali kwa matibabu madhubuti. Kwa mujibu wa Marwa, tatizo la macho katika mkoa wa Iringa ni kubwa, na shirika la KCCO Tanzania limeamua kusaidia kupunguza mzigo huo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Dkt. Jasmine Kachemila, daktari bingwa wa macho kutoka  Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, amesema wamefanya uchunguzi katika kituo cha afya cha Ipogoro na kubaini magonjwa mbalimbali ya macho ikiwemo mtoto wa jicho, presha ya macho na matatizo yanayohusiana na uvaaji wa miwani. Amesema changamoto kubwa ni kwamba watu wengi wanaumwa, lakini hawafiki hospitali. Baadhi hutumia dawa bila ushauri, jambo linaloongeza hatari ya kupoteza uono.

Ameeleza kuwa wagonjwa waliogundulika na mtoto wa jicho watapelekwa katika hospitali ya rufaa kwa ajili ya upasuaji kwa gharama nafuu, kwa kushirikiana na wataalamu na wafadhili wa KCCO Tanzania.

Naye Musa Nzingo, Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Ipogoro, amesema wananchi wamepokea huduma hizo kwa mwitikio mkubwa na kwa furaha, kwani zimewasaidia kupata matibabu ambayo hapo awali walikosa kwa muda mrefu. Ameshukuru Wizara ya Afya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na shirika la KCCO Tanzania kwa kuboresha huduma za macho na kuwafikia wananchi hadi maeneo ya ndani.

Baadhi ya wananchi walionufaika na huduma hizo akiwemo Chelestina Kabogo wa Ipogoro, wamesema huduma hizo zimekuwa mkombozi mkubwa kwao. Wamewataka wananchi wengine kujitokeza kwa wingi pindi wanaposikia uwepo wa huduma, ili kuepuka kupoteza uwezo wa kuona kutokana na kuchelewa kutafuta matibabu.

Huduma hizo zimeendelea kuleta matumaini makubwa, na wadau wa afya wanaeleza kuwa zina uwezo wa kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa magonjwa ya macho katika mkoa wa Iringa.