Na John Walter-Mbulu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Wilaya ya Mbulu mkoani Mbulu , ambapo imeeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wa Dambia–Haydom.

Akiwasilisha taarifa mbele ya kamati hiyo, Meneja wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini Mkoa wa Manyara, Mhandisi James Kionaumela amesema mradi wa maji wa Dambia–Haydom wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 41 umefikia asilimia 44.5 ya utekelezaji.

Amesema mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Mbulu kwa asilimia 18.7, hali itakayofanya kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 98.7 kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Kwa mujibu wa Kionaumela, mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 2 Novemba 2027 na unakadiriwa kunufaisha zaidi ya wananchi laki moja katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mheshimiwa Jackson Kiswaga, amesema ameridhishwa na maendeleo ya mradi huo na kuipongeza RUWASA kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wake.

Aidha ameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha wananchi wanasogezewa huduma ya maji safi na salama karibu na makazi yao.

Mheshimiwa Kiswaga pia amewahimiza wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kulinda vyanzo vya maji visikauke, huku akiwataka kuongeza ushirikiano katika kulinda miundombinu ya maji na kuepuka vitendo vya uharibifu.

Kwa upande wake, mjumbe wa kamati hiyo na Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, Mheshimiwa Asya Omar, ameshauri katika utekelezaji wa mradi huo kuwepo maeneo maalum ya mifugo kunywa maji ili kupunguza migongano kati ya matumizi ya maji kwa binadamu na mifugo.

Awali kamati hiyo ilipokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, ambapo ameahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wananchi katika kulinda na kuhifadhi vyanzo vya maji ili miradi hiyo iwe na manufaa ya kudumu.

Wananchi waliojitokeza kushuhudia ziara ya kamati hiyo wameishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi huo wakisema kuwa upatikanaji wa maji umekuwa changamoto kubwa kwa muda mrefu na wanaamini mradi huo utaleta suluhisho la kudumu.