Baadhi ya viongozi wa Chama cha msingi cha ushirika Lugari Amcos wakiangalia matumizi ya kompyuta kwa wanafunzi wa shule ya msingi Lugari,Chama hicho kimetumia zaidi ya Sh.milioni 2 kukarabati darasa moja kwa ajili ya somo la kompyuta katika shule hiyo
Na Mwandishi Wetu, Mbinga,
CHAMA cha msingi cha ushirika Lugari kilichopo kata ya Mkumbi Halmashauri ya wilaya Mbinga,kimetumia sehemu ya mapato yake yanayotokana na ushuru wa zao la kahawa kukarabati darasa moja katika shule ya msingi Lugari kwa ajili ya wanafunzi kusoma masomo ya kompyuta.
Katibu wa Lugari Amcos Cornas Kapinga alisema,chama kimetumia zaidi ya
Sh.milioni 2 kwa ajili ya ukarabati wa darasa hilo ambazo ni muendelezo wa Chama hicho kutekeleza takwa la kisheria kwa kurudisha faida kwa jamii(CSR)ambapo kila mwaka kinatenga fedha kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi inayotekelezwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali yao.
Kapinga alisema,darasa hilo lilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi hivyo Amcos imekamilisha kwa kupaka rangi,kufunga madirisha ya aluminiam na kuweka mashine ya kutolea kopi yenye thamani ya shilingi laki tano(500,000) ili kuwawezesha wanafunzi kuwa na uelewa zaidi ya masuala ya kompyuta.
Alisema,katika kata ya Mkumbi yenye shule za msingi zaidi ya sita ni Lugari pekee inayofundisha somo hilo ambalo litawasaidia wanafunzi kufahamu matumizi sahihi ya kompyuta na hatimaye kufanya vizuri kwenye masomo yao.
Aidha alisema,Chama kimeboresha mradi wa maji safi na salama kwa kuweka tenki la lita 2,000 kwa ajili ya kusambaza huduma ya maji safi kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi na walimu wa shule hiyo na kwenye nyumba za walimu.
Alisema,mradi huo umesaidia kuboresha suala la usafi wa madarasani,vyoo na kupikia na wanafunzi wanapata muda mwingi kuwa darasani ikilinganisha na hapo awali ambapo walitumia muda mwingi kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vingine hivyo kupoteza muda wa masomo.
Kwa mujibu wa Kapinga,Lugari Amcos itaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kusaidia huduma za kijamii hususani miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali ili kuboresha huduma muhimu za kijmii.
Mwalimu wa shule hiyo Erasto Kifalu alisema,masomo ya kompyuta yatawasaidia sana wanafunzi katika ujifunzaji wa mfumo wa kisasa wa kidigitali na siyo kwa wanafunzi wa shule hiyo tu bali hata wanafunzi wa shule jirani katika kata ya Mkumbi.
Mwalimu Kifalu,amekipongeza Chama cha msingi Lugari Amcos kwa ukarabati huo kwani wanafunzi watajifunza masomo ya kompyuta,kupata maarifa na kusaidia jamii kupata huduma ya kuchapa taarifa mbalimbali badala ya kwenda Mbinga mjini kufuata huduma hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Veronica Matenga alisema,kuanzishwa kwa somo la kompyuta kutawasaidia kufanya vizuri kwenye masomo yao na kurahisishia walimu kuandaa mitihani na vipindi vya masomo kama ilivyo kwenye shule za mjini.
Mtenga,ameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Mbinga kutoa kompyuta hizo na Chama cha msingi cha ushirika Lugari kutumia sehemu ya mapato yake kufanya ukarabati wa darasa, kufunga mashine ya kutolea nakala(Photocopy) na kuboresha huduma ya maji safi ambayo yamemaliza kero ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama shuleni hapo.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha Lugari Imani Komba(Dae),amekishukuru Chama hicho kwa moyo wa uzalendo kutumia sehemu ya fedha inazopata kurudisha kwa jamii k ambapo amevitaka vyama vingine vya ushirika kuiga mfano wa Lugari Amcos.
Komba alisema,Lugari Amcos imefanya jambo la kupongezwa kwa kuwa kupitia fedha wanazotenga sasa wilaya ya Mbinga itafanya vizuri kwenye elimu hivyo kupata wasomi wengi kutoka vijijini ambao watakwenda kuhudumia wananchi kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo sekta ya afya
Baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Lugari kata ya Mkumbi Halmashauri ya wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma wakiendelea na masomo kwa kutumia kompyuta kama sehemu ya kuwajengea uelewa zaidi kwenye masomo yao.
