Katibu Tawala wa wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Francis Mgoloka kushoto,akipokea mashine kwa ajili ya kusaidia matatizo ya upumuaji kwa watoto wachanga kutoka kwa Meneja shughuli wa kampuni ya Premium Active Tanzania Nicco Rousous kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya Namtumbo.Baadhi ya wafanyakazi wa kampuni ya Premium Active Tanzania Mkoa wa Ruvuma,wakifuatilia zoezi la ugawaji wa vifaa tiba na michezo vilivyotolewa na kampuni hiyo kwa ajili ya kutatua changamoto ya upumuaji kwa watoto wachanga katika Hospitali ya wilaya Namtumbo.

Na Mwandishi Wetu,Namtumbo

KATIBU Tawala wa wilayani Namtumbo Francis Mgoloka,amezitaka Taasisi na makampuni yote yanayofanya shughuli zake katika wilaya hiyo,kutimiza takwa la kisheria kwa kurudisha sehemu ya faida(CSR) inazopata kuchangia kwenye miradi ya maendeleo ili kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo afya na elimu.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma Francis Mgoloka,alipokuwa akipokea msaada wa mashine moja ya kusaidia upumuaji(CPAP Machine) kwa watoto wadogo na wanaozaliwa kabla ya wakati(Njiti) na vifaa mbalimbali vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 10 kutoka kwa kampuni ya Premium Active Tanzania inayonunua tumbaku wilayani Namtumbo.

Mgoloka,amezitaka kampuni zote kuona namna ya kurudisha faida wanayopata katika kuhudumia jamii na kusaidiana na serikali iliyopo madarakani katika kuboresha huduma mbalimbali ambazo zitachochea na kuharakisha kwa maendeleo kwa wananchi.

Mgoloka,ameishukuru kampuni ya Premium Active Tanzania kwa kuweza kufanikisha upatikanaji wa mashine hiyo ambayo inakwenda kuokoa maisha ya watoto wengi wanaozalisha wakiwa na tatizo la upumuaji na kusaidia ukuaji kwa watoto njiti ambao wanahitaji uangalizi wa karibu kwa kumia mashine na wataalam wa afya.

“Sisi kama serikali tutaendelea kushirikiana na nyinyi kuhakikisha mnafanikisha malengo yenu ya kuinua kilimo cha zao la tumbaku na wakulima wanaongeza uzalishaji wa zao hilo mwaka hadi mwaka”alisema Mngoloka.

Kwa upande wake Meneja shughuli wa kampuni ya Premium Active Tanzania Nicco Rousous alisema,wataendelea kuchangia huduma za jamii na miradi ya mendeleo kwenye maeneo yote yanayozalisha zao la tumbaku kwani wao ni wadau wa kweli wa maendeleo hapa nchini.

Alisema,katika kufanikisha takwa hilo la kisheria kampuni ilipokea miradi ya kipaumbele kutoka kwenye kata zenye vyama vya ushirika vya msingi vinavyofanya kazi na kampuni ya Premium.

Aidh alisema,kampuni ya Premium Active Tanzania imetoa vifaa vya michezo kwa shule ya sekondari Nasuli na makabati ya kutunzia nyaraka kwa ajili ya ofisi ya serikali ya kijiji cha Matiri wilayani Mbinga vyote vikiwa na thamani ya Sh.milioni 10.9.

Alisema,kampuni hiyo imekuwa na utaratibu huo kwenye Halmashauri nane za mikoa mitano hapa nchini inafanya kazi na Premium Active Tanzania na inachangia madawati,visima vya maji,vifaa vya Hospitali na michezo vyeny jumla ya Sh.162,832,737.06 na uchangiaji huo unaendena na uzalishaji wa kata au Halmashauri husika.

“Ni vigumu kukidhi mahitaji yote ya kila eneo,lakini kutoa mashine hii na vifaa vya michezo tunaamini tumetimiza wajibu wetu kama kampuni kwa kuchangia katika maendeleo ya afya na michezo katika wilaya ya Namtumbo”alisema.

Mwakilishi wa Mganga mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sosthenes Mumba alisema,mashine hiyo inakwenda kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati(njiti)na watoto wachanga wenye changamoto ya upumuaji.

Alisema,katika Hospitali ya wilaya kuna mashine mbili ambazo hazitoshelezi mahitaji kutokana na ongezeko kubwa la watoto wanaozaliwa wakiwa na changamoto hizo,hivyo walilazimika kuwasafirisha kwenda Hospitali ya Mkoa Songea mjini au Hospitali ya misheni Peramiho na mashine hiyo itasaidia kuongeza nguvu na kupunguza kasi ya kusafirisha wagonjwa kwenda maeneo mengine nje ya wilaya ya Namtumbo kwa ajili ya kufuata huduma hizo.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wa zao la Tumbaku wa wilaya ya Namtumbo Juma Mwanga alisema,kampuni ya Premium Active Tanzania ndiyo pekee inayonunua tumbaku katika Halmashauri ya wilaya Namtumbo ambayo tangu ilipoanza shughuli zake ndiyo iliyoonyesha mwitikio wa kurudisha faida inayopata kwa jamii.

Alisema,wakulima wa tumbaku ni wazazi wenye watoto hivyo mashine hiyo itasaidia sana kuokoa maisha ya watoto wao na wazazi kupata muda mwingi zaidi wa kujikita kwenye kilimo cha tumbaku badala ya kwenda Hospitali mara kwa mara kufuata huduma za watoto wao.

Alisema,hatua ya Premium kurejesha faida kwa jamii inatengeneza mahusiano mazuri kati ya kampuni hiyo,wakulima na jamii ya wana Namtumbo ambayo zaidi ya asilimia 85 wanategemea zao la tumbaku kama nguzo kuu ya uchumi wao.

“kwa niaba ya wakulima wenzangu wa Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla tunatendelea kuzalisha tumbaku bora ili kukidhi mahitaji ya kampuni ya Premium,natoa wito kwa makampuni mengine yanayonunua tumbaku katika mkoa

wetu waige mfano mzuri wa Premium kwa kurudisha faida wanayopata badala ya kutunyonya na kuondoka”alisema Mwanga.