NA DENIS MLOWE, MAFINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewahimiza wanawake na wasichana kujitokeza kwa ujasiri kushiriki kikamilifu katika nyanja za uongozi, uchumi na maendeleo ya jamii ili kuimarisha familia, jamii na taifa kwa ujumla.
Akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake yaliyofanyika kimkoa wilaya Mufindi katika Ukumbi wa Mamu, Kheri alisema wanawake tayari wanaonesha uwezo mkubwa katika nafasi mbalimbali za uongozi ikiwemo urais, ubunge, udiwani na uongozi wa taasisi na mashirika, huku pia wakifanya vizuri katika shughuli za kiuchumi.
Alisema wanawake wengi wamefanikiwa kumiliki makampuni, taasisi na biashara mbalimbali, hali inayoonesha mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa jamii na taifa.
Pamoja na mafanikio hayo, Kheri alieleza kuwa bado wapo wanawake na wasichana wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fursa sawa katika elimu na ajira, vitendo vya ukatili wa kijinsia, uwakilishi mdogo katika nafasi za maamuzi pamoja na mzigo mkubwa wa majukumu ya familia na malezi.
Aliongeza kuwa umiliki mdogo wa ardhi na rasilimali nyingine kwa wanawake ukilinganisha na wanaume pia ni changamoto inayohitaji juhudi za pamoja kutoka kwa jamii na serikali.
Alisema serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ili kuwawezesha wanawake kujisimamia kiuchumi na kunufaika na fursa zilizopo kupitia sera, sheria na programu mbalimbali zinazolinda na kutetea haki za wanawake.
Kheri alifafanua kuwa miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kutungwa kwa sera na sheria zinazolenga kuimarisha usawa wa kijinsia, kuboresha upatikanaji wa elimu kwa wasichana na wanawake pamoja na kuanzishwa kwa programu mbalimbali za mafunzo ya ufundi ili kuwapa ujuzi utakaowasaidia kujitegemea kiuchumi.
Aidha alitaja juhudi zinazofanywa katika kuboresha huduma za afya kwa wanawake hususan huduma za afya ya uzazi, huduma kwa mama na mtoto pamoja na kampeni za kupunguza vifo vya wajawazito.
Alisema serikali pia imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia ya mawasiliano ili kuwasaidia wanawake kufikia masoko, kufanya biashara mtandaoni na kuongeza ujuzi wa kidijitali kwa wanawake wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali.
Mkuu huyo wa mkoa aliitaka jamii kuendelea kuwahamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi kwani kuwapa wanawake nafasi ya kushiriki katika maamuzi kunachangia kujenga familia imara, jamii imara na taifa imara.
Katika hotuba yake pia aliwahimiza wazazi kuachana na dhana potofu zinazodhoofisha maendeleo ya mtoto wa kike, akisisitiza kuwa wasichana wana uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika elimu, kazi na uongozi kama walivyo wavulana.
Alisema wanawake wengi tayari wameonyesha uwezo mkubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, utawala, siasa na biashara na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Mkoa wa Iringa.
Kwa upande mwingine alisisitiza umuhimu wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuhakikisha wahusika wa vitendo hivyo wanachukuliwa hatua za kisheria.
Aliongeza kuwa ushahidi na ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha kesi za ukatili zinachunguzwa na wahusika kuchukuliwa hatua ili kulinda haki na usalama wa wanawake na watoto.
Mwisho, Kheri aliwataka wanawake kujiamini, kutumia vipaji na uwezo wao katika kujiletea maendeleo na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Katika maadhimisho hayo Mkuu wa mkoa wa Iringa aliongoza zoezi la kutoa zawadi kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Fiderica Myovela kutokana na utendaji kazi wake ambapo wanawake wa mkoa wa Iringa walijipanga kumtunza kwa kukubalika kwake.