Wanawake kutoka Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) wakiwa katika Maandamano ya Kuadhimisha siku  Wanawake Duniani yaliyofanyika leo Machi 8, 2026, Mburahati, Viwanja vya Barafu, Dar es Salaam.

…….

Wanawake kutoka Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji Umeme (ETDCO) wameungana na wanawake wengine duniani kusherehekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika leo Machi 8, 2026, Mburahati, Viwanja vya Barafu, Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yameongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, yakiwakutanisha wanawake kutoka taasisi mbalimbali za serikali na binafsi, yakilenga kuadhimisha mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika chini ya kauli mbiu isemayo: “Haki kwa wanawake na wasichana ni msingi wa maendeleo jumuishi kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki na fursa sawa katika elimu, uchumi na uongozi, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa katika kufanikisha maendeleo endelevu ya taifa.

Kupitia maadhimisho hayo, washiriki wamepata fursa ya kujadili namna ya kuendelea kuimarisha usawa wa kijinsia na kuhamasisha jamii kushiriki katika kuondoa vikwazo vinavyoweza kuzuia maendeleo ya wanawake na wasichana nchini.