NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, ameshiriki futari pamoja na watoto wanaolelewa katika Kituo cha Yatima cha Bilal na Fatma kilicho chini ya Taasisi ya Dhinureyne, huku akiahidi kusaidia kutatua baadhi ya changamoto zinazolikabili kituo hicho.
Akizungumza wakati wa futari hiyo, Ngajilo alisema amefurahi kupata nafasi ya kushiriki chakula hicho na watoto hao, akisisitiza kuwa anawaona kama ndugu na sehemu ya familia yake.
Alisema kuwa amekuwa na utamaduni wa kutembelea vituo vya watoto yatima kila mwaka, na mwaka huu aliamua kurejea tena katika kituo hicho ili kuendeleza mshikamano na kuwapa faraja watoto wanaolelewa hapo.
Mbunge huyo alieleza kuwa dua za watoto hao zilikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio yake ya kisiasa, akiwashukuru kwa kumuombea hadi akapata nafasi ya kuwa mbunge.
“Dua zenu zimekuwa dua zilizosikilizwa. Nawaomba muendelee kutuombea sisi viongozi ili tuweze kutumikia jamii vizuri,” alisema.
Ngajilo alisema amesikia changamoto mbalimbali zinazolikabili kituo hicho na kuahidi kuzifanyia kazi kwa kushirikiana na wasaidizi wake pamoja na mamlaka za serikali.
Alitaja moja ya changamoto hizo kuwa ni ukosefu wa mfumo wa nishati ya sola, akieleza kuwa kituo hicho kinatumia umeme mwingi kuendesha mota ya kupandisha maji kutoka kwenye kisima, hali inayosababisha gharama kubwa za umeme.
Alisema suala hilo amelichukua kama jukumu lake na ameahidi kulifanyia kazi ili kusaidia kupunguza gharama kwa kituo hicho.
Mbali na hilo, Ngajilo alizungumzia changamoto ya barabara inayoelekea kituoni hapo, akisema atashirikiana na viongozi wa serikali katika ngazi ya wilaya, kata na wataalamu ili kuona namna bora ya kuboresha miundombinu hiyo.
Aidha, alieleza kuwa watoto walioko kituoni hapo wameomba mipira ya michezo, jambo ambalo alisema halihitaji mchakato mrefu.
Alisema tayari amemuagiza katibu wake kuhakikisha watoto hao wanapatiwa mipira ya kuchezea ifikapo siku inayofuata.
Katika hatua nyingine, Ngajilo alitoa wito kwa jamii na Watanzania kwa ujumla kuendelea kutembelea na kusaidia vituo vya watoto yatima kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo chakula na mahitaji mengine muhimu.
Alisema hata msaada mdogo kama kilo moja ya unga unaweza kuwa na thamani kubwa kwa watoto hao na kusaidia kuboresha maisha yao.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuwa na mkakati wa kitaifa wa kumaliza kabisa tatizo la watoto wa mitaani, akisema jamii ina wajibu wa kushirikiana kuhakikisha watoto wote wanapata malezi bora.
“Niko tayari kama mbunge kushirikiana na wadau wote wenye mawazo mazuri yatakayosaidia kumaliza kabisa tatizo la watoto wa mitaani ili libaki kuwa historia,” alisema.
Kwa upande wake, msimamizi mkuu wa kituo hicho, Hanifa Omary, alimshukuru mbunge huyo kwa kutembelea kituo hicho na kushiriki futari pamoja na watoto.
Alisema kwa sasa kituo hicho kinahudumia takribani watoto 50, huku watoto 20 wakipokelewa mwezi Desemba mwaka jana.
Aliongeza kuwa watoto wengine 15 waliomaliza kidato cha nne wapo nyumbani kwa sasa baada ya kumaliza masomo yao, huku matokeo yao yakiwa mazuri ikiwemo baadhi kupata daraja la kwanza, la pili na la tatu.
Omary alisema licha ya mafanikio hayo, kituo hicho kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo hitaji la mfumo wa sola kwa ajili ya mota ya maji pamoja na ubovu wa barabara inayoelekea kituoni hapo.
Alisema ubovu wa barabara hiyo umekuwa ukileta changamoto kwa watoto wanapoenda na kurudi shuleni, na pia kwa wageni wanaotaka kufika kutoa misaada.
“Watu wengine wanaogopa kuja kuleta misaada kwa sababu ya hali mbaya ya barabara, wakihofia magari yao kuharibika,” alisema.
Hata hivyo, alimshukuru mbunge huyo kwa ahadi alizotoa na kusema wana imani kuwa zitasaidia kuboresha mazingira ya kituo hicho pamoja na ustawi wa watoto wanaolelewa hapo.

