Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Machi 07, 2026 ameshiriki katika Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika jijini Arusha.
Mkutano huo uliwakutanisha Marais Mhe. William Samoei Ruto wa Jamhuri ya Kenya; Mhe. Évariste Ndayishimiye wa Jamhuri ya Burundi; Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wa Jamhuri ya Uganda; na Mhe. Hassan Sheikh Mohamud wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia. Aidha, Jamhuri ya Rwanda iliwakilishwa na Waziri Mkuu Mhe. Justin Nsengiyumva kwa niaba ya Rais Paul Kagame, huku Jamhuri ya Sudan Kusini ikiwakilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Balozi Monday Semaya Kumba kwa niaba ya Rais Salva Kiir Mayardit.
Pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo iliwakilishwa na Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda Mhe. Didier Mazenga Mukanzu kwa niaba ya Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, ambapo viongozi hao walikutana kujadili maendeleo ya ushirikiano wa kikanda, biashara na ustawi wa wananchi wa Afrika Mashariki.
Katika mkutano huo, Wakuu wa Nchi Wanachama wamemteua Balozi Steven Patrick Mbundi wa Tanzania kuwa Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa kipindi cha miaka mitano kisichoweza kuongezwa.

