
Wafanyakazi wa Benki ya NMB Bank Plc wakiwa katika ziara ya kutembelea miradi ya makazi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ikiwemo mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi pamoja na Kawe 711 iliyofanyika leo Machi 7, 2026 Jijini Dar es Salaam.
……….
Wafanyakazi wa Benki ya NMB Bank Plc wametembelea miradi ya makazi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), ikiwemo mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi pamoja na Kawe 711, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano katika kuwawezesha Watanzania kumiliki nyumba kupitia mikopo ya benki.
Akizungumza leo Machi 7, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara hiyo, Meneja Mahusiano wa Mikopo ya Nyumba wa Benki ya NMB, Pauline Sangale, amesema kuwa nyumba zinazojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa zina ubora wa hali ya juu.
Ameeleza kuwa benki hiyo inatoa hadi asilimia 90 ya mkopo wa nyumba ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki makazi.
Aidha, ameipongeza NHC kwa juhudi zake za kuboresha makazi nchini pamoja na kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nyumba inayouzwa kwa bei rafiki kwa wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Bw. Thobias Kavishe, amesema kuwa miradi hiyo imetoa fursa za uwekezaji wa aina tatu za nyumba, ikiwemo nyumba za vyumba viwili, vitatu na vinne ambazo zinauzwa kwa bei nafuu.
“Tunatoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa za nyumba zinazojengwa na NHC. Mnunuzi anaweza kupata nyumba kupitia njia tatu ikiwemo kulipa fedha taslimu, kupitia mikopo ya benki washirika, au kufanya malipo ya awamu ndani ya kipindi cha ujenzi,” amesema Bw. Kavishe.
Katika ziara hiyo, timu ya NMB ilipata fursa ya kujionea maendeleo ya miradi ya makazi ya kisasa inayotekelezwa na NHC, ikiwemo mradi wa Samia Housing Scheme Kijichi pamoja na Kawe 711, miradi inayolenga kuongeza upatikanaji wa nyumba bora zenye miundombinu ya kisasa kwa wananchi.
Maafisa wa benki hiyo pia walipatiwa maelezo kuhusu ubora wa ujenzi wa miradi hiyo, huduma zitakazopatikana pamoja na mifumo ya malipo inayowawezesha wananchi kununua nyumba hizo, ikiwemo mfumo wa mkopo wa nyumba (mortgage) unaotolewa kupitia benki washirika.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni hatua muhimu ya kuimarisha ushirikiano kati ya NHC na sekta ya benki, kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya nyumba na hivyo kuwasaidia Watanzania wengi zaidi kumiliki makazi bora na ya kisasa.
