NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, ameitaka jamii kutafakari na kuchambua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake ili kutafuta suluhisho na hatimaye kujenga maisha bora kwa wote.
Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka Machi 8 kwa halmashauri ya manispaa Iringa iliyofanyika katika uwanja wa Samora, Sitta alisema siku hiyo ni fursa muhimu kwa serikali na wadau mbalimbali kutathmini utekelezaji wa sera, programu na mikakati inayolenga kuleta usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana.
Alisema kuwa kufikiwa kwa usawa wa kijinsia kunahitaji ujasiri, ubunifu na elimu pamoja na kupambana na ubaguzi na kutengwa kwa wanawake katika jamii.
Sitta alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za kifedha imeendelea kutoa mafunzo, mikopo na mitaji kwa wanawake ili waweze kuanzisha na kuendeleza miradi midogo ya kiuchumi.
Alisema miradi hiyo husaidia kuongeza kipato cha wanawake na kuwawezesha kumudu gharama za maisha ya kila siku pamoja na kuleta maendeleo katika familia na jamii kwa ujumla.
Aidha alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kusisitiza utolewaji wa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya halmashauri inayotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Alisema Manispaa ya Iringa imekuwa kinara katika utoaji wa mikopo hiyo na kuwataka wanawake kutumia fursa hiyo kwa kujiunga katika vikundi na kujisajili ili waweze kunufaika na fedha hizo.
Sitta pia alitaja taasisi na mashirika mbalimbali yanayosaidia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi ikiwemo FINCA, IDYDC, Faidika, BRAC, SIDO na ASA ambazo zimekuwa zikitoa mikopo pamoja na mafunzo ya ujasiriamali.
Alifafanua kuwa wanawake wengi wamejikita katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo biashara ndogondogo, ufugaji wa kuku, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, uuzaji wa samaki, utengenezaji wa keki, upambaji wa sherehe pamoja na vikundi vya kuweka na kukopa.
Alisema shughuli hizo zimekuwa zikilenga kumwezesha mwanamke kiuchumi ili aweze kujitegemea na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii sambamba na malengo ya maendeleo ya taifa.
Katika hatua nyingine, Sitta alisema elimu kuhusu ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono imetolewa kwa wanawake katika wiki ya maadhimisho hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Alisema takwimu zinaonyesha kuwa wanawake wengi bado wanakumbwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikilinganishwa na makundi mengine, huku watoto pia wakiwa miongoni mwa waathirika.
Kutokana na hali hiyo aliwataka wanawake kujitokeza kutoa taarifa pindi vitendo vya ukatili vinapotokea ili vyombo vya sheria viweze kuchukua hatua stahiki.
Alisema mara nyingi kesi nyingi hushindwa kufikia hatua za kisheria kutokana na wahanga au mashahidi kushindwa kutoa ushirikiano au kuamua kumaliza migogoro kienyeji.
Pia alionya kuhusu matukio ya udanganyifu katika mahusiano ambapo baadhi ya wanawake wamekuwa wakimiliki mali kwa watu wanaowaamini bila kufuata taratibu za kisheria, jambo linalosababisha migogoro mingi baadaye.
Aliwataka wanawake kuwa makini katika masuala ya mahusiano na kufuata taratibu sahihi hasa katika ndoa ili kuepusha migogoro ya mali na haki za kifamilia.
Sitta pia alizungumzia umuhimu wa malezi bora kwa watoto akieleza kuwa mabadiliko ya teknolojia na matumizi ya mitandao yanaathiri maadili ya jamii, hivyo wazazi wanapaswa kuzingatia malezi, lishe bora na maadili kwa watoto.
Alisema lishe bora ni muhimu katika kupambana na matatizo ya utapiamlo na udumavu kwa watoto.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Iringa, Zaina Mlawa alisema wanawake wa Manispaa ya Iringa walitumia wiki nzima ya maadhimisho kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa pamoja na michezo na mijadala ya maendeleo.
Alisema shughuli hizo ziliwapa wanawake fursa ya kujifunza, kubadilishana mawazo na kukumbushana majukumu yao katika familia na jamii.
Aidha alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Iringa pamoja na viongozi wengine wa serikali na wadau kwa kushiriki na kuunga mkono shughuli za wanawake katika kipindi chote cha maadhimisho hayo.
Mlawa alisema wanawake wanaendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo huku wakitimiza majukumu yao katika familia kama mama na wake.
Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wanawake na wanaume ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya jamii.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, amewahimiza wanawake wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kushiriki semina za ujasiriamali zinazoandaliwa na ofisi yake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha.
Ngajilo alisema lengo la semina hizo ni kuwajengea wanawake uwezo wa kufanya biashara, kuweka akiba na kutumia fursa za mikopo ili kujikwamua kiuchumi.
Alisema semina ya kwanza ilifanyika mapema mwaka huu na kuhudhuriwa na zaidi ya wanawake 100, huku semina inayofuata ikitarajiwa kufanyika mwezi wa tano mwaka huu na kulenga kushirikisha takribani wanawake 500.
Ngajilo alifafanua kuwa zoezi la kujiandikisha kwa washiriki litaanza mwezi wa nne, ambapo wanawake watatakiwa kuacha majina na mawasiliano yao ili kurahisisha uratibu wa mafunzo hayo.
Aidha, alibainisha kuwa taasisi za fedha zikiwemo Azania Bank na wadau wengine zitashiriki kutoa elimu ya fedha na mbinu za uwekezaji mdogo kwa wanawake. Alisema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuongeza uelewa wa ujasiriamali kwa wanawake wa Iringa Mjini kupitia semina zitakazokuwa zikifanyika mara kadhaa kila mwaka.