Na John Walter-Manyara

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Regina Ndege ametoa msaada wa vitimwendo 10 kwa watu wenye mahitaji maalum, hususan wenye ulemavu wa viungo, ikiwa ni sehemu ya kuwasaidia kurahisisha maisha yao ya kila siku.

Akikabidhi msaada huo, Regina amesema kuwa kila anapopata nafasi au uwezo mdogo wa kusaidia, huwa anawakumbuka watu wenye mahitaji maalum kwa kuwa wanahitaji msaada na uangalizi zaidi kutoka kwa jamii.

Amesema hatua hiyo pia ni sehemu ya kumuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye amesema amekuwa mstari wa mbele kusaidia na kutetea haki za makundi yenye mahitaji maalum katika jamii.

Aidha, Regina amesema vitimwendo hivyo vitasaidia kupunguza mzigo kwa wazazi na walezi ambao hulazimika kuwabeba watoto wenye ulemavu wanapokwenda shule au katika shughuli nyingine za kijamii.

Amewataka walionufaika na msaada huo kuvithamini na kuvitunza vizuri ili viweze kuwasaidia kwa muda mrefu, huku akisisitiza jamii kutowaficha watu wenye mahitaji maalum bali kuwapa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

Pia ametoa wito kwa watu wengine wenye uwezo kujitokeza na kuwakumbuka watu wa aina hiyo kwa kuwasaidia mahitaji yao mbalimbali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Babati Mjini, Eva Makilagi ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum, amempongeza Regina Ndege kwa moyo wake wa kujitoa kusaidia jamii na kuwataka viongozi na wadau wengine kuiga mfano huo.

Baadhi ya walionufaika na msaada huo wamemshukuru Regina Ndege wakisema vitimwendo hivyo vitawasaidia kurahisisha maisha yao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za elimu na kijamii.