Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amesema maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa ngazi ya Mkoa wa Dodoma mwaka 2026 yatafanyika katika Wilaya ya Kongwa Machi 8, 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Mbande.
Aidha amesema katika kuelekea maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika kupitia vituo mbalimbali vya redio, kupanda miti katika Kata ya Kikuyu Kusini, ugawaji wa majiko banifu kwa wananchi wa Chamwino Kata ya Mlowa, mdahalo wa wanawake katika ukumbi wa Chimwaga Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kufanya matendo ya huruma katika shule zenye mahitaji Kondoa TC, kongamano la wanawake wa elimu Bahi DC pamoja na kongamano la Umoja wa Wanawake wa Kikristo katika Kata ya Kizota.
Rc Senyamule ameyasema hayo Machi 6, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma.
Amesema kuwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yalianza mwaka 1911 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta ya viwanda nchini Marekani waliopinga mazingira duni ya kazi ikiwemo ukosefu wa huduma za kijamii na vitendo vya unyanyasaji katika ajira pamoja na wanawake kulipwa mishahara midogo kwa kazi sawa na zile za wanaume.
Aidha amebainisha kuwa uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuadhimisha siku hiyo ulitokana na ukweli kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa kijinsia yalihitaji msukumo maalum wa kipekee kutoka kwa jamii husika.
Pia ameongeza kuwa nchini Tanzania Siku ya Wanawake Duniani ilianzishwa mwaka 1997 ambapo Serikali ilipitisha uamuzi wa maadhimisho hayo kufanyika kitaifa kila baada ya miaka mitano na kila mwaka kufanyika katika ngazi ya mikoa na wilaya.
Amesema lengo la utaratibu huo ni kutoa muda wa utekelezaji wa maazimio pamoja na kupima mafanikio yaliyofikiwa.
Amesema kufanya mzunguko wa maadhimisho hayo katika halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Dodoma kunalenga kutoa fursa kwa wanawake wa vijijini kushiriki maadhimisho hayo ili kujifunza na kujadili masuala yanayohusu uwezeshaji wa wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Aidha amebainisha kuwa katika siku tatu za maadhimisho hayo kutakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo maonyesho ya huduma na bidhaa kutoka wizara 27, taasisi mbalimbali, mashirika na makampuni binafsi na ya umma, taasisi za kimataifa pamoja na taasisi zisizo za kiserikali.
Amebainisha kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka 2026 inasema “Haki na usawa kwa wanawake na wasichana, msingi jumuishi kufikia Dira ya 2050.”
Amesema kauli mbiu hiyo inalenga kujenga uelewa kwa jamii na wadau kuwekeza katika maendeleo jumuishi kwa kutambua haki za wanawake na wasichana na kuhakikisha zinafanyiwa kazi kwa vitendo ili kuleta mabadiliko ya kweli kama ilivyoainishwa katika nguzo za Dira ya 2050.
Pia ameongeza kuwa kuanzia Machi 6 hadi Machi 8 kutakuwa na maonyesho ya wadau mbalimbali pamoja na wajasiriamali kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Dodoma kujitangaza na kuuza bidhaa zao, sambamba na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria, elimu pamoja na huduma za kibenki.
Pia,Rc Senyamule ametoa wito kwa wananchi kutumia fursa hiyo ambayo itawakutanisha zaidi ya washiriki elfu sita kujifunza mambo mbalimbali pamoja na kutangaza huduma na bidhaa zao ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

