Katibu wa afya wa Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma George Mhina kushoto,akikagua njia za watembea kwa miguu katika Hospitali ya Hamashauri hiyo iliyopo eneo la Hifadhi kata ya Kigonsera,kulia Mganga Mfawidhi Dkt Salum Bundala.

Wodi ya upasuaji katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

Muonekano wa jengo la dharura(ICU) katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma kama linavyoonekana.

…………..

Na Mwandishi Maalum, Mbinga

KATIBU wa afya Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma George Mhina amesema,kukamilika kwa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Halmashauri hiyo iliyopo eneo la hifadhi litamaliza changamoto kwa wananchi waliokuwa wakikosa huduma ya upasuaji na kukimbilia Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mbinga au Hospitali ya Rufaa ya Songea.

Mhina alisema kuwa,jengo hilo lililogharimu Sh.milioni 350 lilianza kujengwa mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia mkandarasi kwa gharama ya Sh.milioni 299,580,874 na mkandarasi amemaliza kazi zote kwa mujibu wa mkataba wake na amelipwa Sh.milioni 284 na fedha iliyobaki italipwa baada ya kumalizika kwa kipindi cha matazamio.

Mhina alisema,ujenzi wa jengo hilo umekamilika kwa asilimia mia moja na Serikali kupitia Halmashauri ipo kwenye mchakato wa kufunga vifaa tiba kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,kwa kuwapatia fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji kwani wanaamini wananchi wa wilaya ya Mbinga watanufaika na huduma ya upasuaji itakayotolewa katika jengo ambalo awali halikuwepo.

Alisema, kukamilika kwa jengo la upasuaji ni mwendelezo wa ujenzi wa majengo ya kisasa katika Hospitali hiyo tangu ilipoanza kujengwa mwaka 2019 wamefikisha jumla ya majengo 13 ambayo yanatoa huduma za afya kwa wananchi.

Mhina alieleza kuwa,jengo hilo kuna vyumba vya upasuaji, ofisi ya wataalamu,chumba cha kutakasia vifaa tiba na wodi ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji na kukamilika kwake litamaliza changamoto kwa wananchi wa Halmashauri hiyo na maeneo mengine ya wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

“Hadi sasa ujenzi wa jengo hili kubwa na la kisasa umekamilika kwa asilimia 100 na tunategemea tutaanza kulitumia kwa kutoa huduma mara baada ya kufika kwa vifaa tiba,tayari serikali imetoa fedha zote na sisi kama Halmashauri kupitia mapato yetu ya ndani tumeagiza vifaa tiba kutoka Bohari ya Dawa(MCD)ili tuanze kuwahudumia wananchi wetu”alisema Mhina.

Kwa mujibu wa Mhina,kukamilika kwa ujenzi huo na upatikanaji wa huduma bora katika Hospitali hiyo itasaidia sana kumaliza changamoto kwa wananchi waliokuwa wakiteseka kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo kwenye Hospitali nyingine.

Aidha alisema,wamepokea jumla ya watumishi wapya 120 wa sekta ya afya na katika Hospitali ya Halmashauri wamepelekwa watumishi 40 ambao wataungana na waliopo kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga Dkt Salum Bundala,ameipongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mradi wa jengo la upasuaji katika Hospitali hiyo, kwani awali halikuwepo na huduma zilizotolewa ni kwa ajili ya akina mama wajawazito kwenye jengo dogo.

“Jengo hili litamaliza kabisa adha kwa wagonjwa ambao ni wanaume wanaohitaji kufanyiwa upasuaji na tunaishukuru Serikali kuajiri watumishi wengi wa kada ya afya na sisi tumepata madaktari 4 wa upasuaji kwa hiyo tutakapofungua jengo hili ni rasmi sasa wagonjwa wetu wanaume watapata huduma kwenye jengo letu jipya”alisema Dkt Bundala.

Mkazi wa kijiji cha Amanimakolo Michela Hyera alisema,kwa sasa changamoto kubwa wanalazimika kwenda maeneo mengine ili kupata huduma ya upasuaji na kuiomba Serikali kuharakisha kuleta vifaa tiba ili waweze kupata huduma kwenye Hospitali ya Halmashauri iliyopo karibu na makazi yao.

Alisema jengo hilo litakapoanza kutoa huduma litakuwa msaada mkubwa kwao kwani litapunguza gharama ya kusafiri kutoka Mbinga hadi Hospitali ya Misheni Peramiho iliyopo Halmashauri ya Wilaya Songea na gharama za matibabu kuwa rahisi kwani Hospitali binafsi zinatoza fedha nyingi.

Helen Aloyce mkazi wa kiijiji cha Matiri,ameishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya wilaya Mbinga kusogeza huduma za afya karibu kwani awali walisafiri kwenda wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma kufuata huduma hizo ambazo kwa sasa zinapatika katika Halmashauri yao.