Wakili wa Serikali , Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Tamari Mndeme, amewaongoza baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Mkoa na wilaya pamoja na Mwakilishi na wanachama wa Chama cha Mawakili wa Serikali Mkoa wa Kilimanjaro, kutembelea wafungwa katika Gereza Kuu la Karanga lililopo katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro
Bi. Tamari amefanya ziara hiyo tarehe 5 Machi, 2026 na kutoa msaada wa kisheria pamoja na mahitaji mbalimbali kwa wafungwa waliopo katika Gereza hilo.
Aidha, amesema kuwa Msaada uliotolewa unajumuisha sabuni za unga, mafuta ya kupaka pamoja na taulo za kike kwa ajili ya wafungwa wanawake.
Katika hatua nyingine, Bi. Tamari ameeleza kuwa hatua hiyo inalenga kuonesha kujali na kuthamini haki na utu wa wafungwa kwa kuwafariji na kuwapatia mahitaji yao ya msingi.
“Licha ya wanawake hawa kuwepo gerezani hakuondoi thamani yao kama ambavyo dhima ya mwaka huu inasisitiza haki na usawa katika kufikia dira ya taifa 2050.” amesema Bi. Tamari
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ,katika Mkoa wa Kilimanjaro kinatarajiwa kufanyika tarehe 8 Machi, 2026 katika Wilaya ya Hai, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu.

