Na Silivia Amandius
Kagera
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera imekamata bidhaa za magendo zenye thamani ya shilingi 57,160,177 katika operesheni maalum iliyofanyika Desemba 2025 kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Missenyi.
Kwa mujibu wa taarifa ya TAKUKURU, operesheni hiyo ilifanyika baada ya kupatikana taarifa za siri kuhusu uwepo wa mizigo iliyokuwa ikiingizwa nchini kutoka Uganda kinyume cha sheria bila kulipiwa kodi stahiki.
Katika msako huo, magari matano yalikamatwa yakiwa yamesheheni bidhaa mbalimbali zikiwemo tani 38 za karanga, tani 16 za karanga, tani 33 za karanga, injini ya gari pamoja na katoni 303 za pombe haramu. Magari hayo yalikuwa yakitumia njia zisizo rasmi kupitisha mizigo hiyo nchini.
TAKUKURU imeeleza kuwa bidhaa hizo zilikuwa zinaingizwa nchini bila kufuata taratibu za forodha, hali inayosababisha upotevu wa mapato ya Serikali na kuathiri uchumi wa taifa.
Bidhaa zote zilizokamatwa zimekabidhiwa kwa vyombo husika kwa ajili ya hatua za kisheria, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Kagera imepokea jumla ya malalamiko 121 yanayohusiana na tuhuma za rushwa katika kipindi hicho. Kati ya hayo, malalamiko 86 yalihusu rushwa, ambapo baadhi ya kesi zimefunguliwa mahakamani na nyingine zinaendelea kuchunguzwa.
Aidha, taasisi hiyo imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa kupitia mikutano ya hadhara, semina na klabu za wapinga rushwa, ambapo zaidi ya wananchi 19,250 wamefikiwa.
TAKUKURU imewataka wananchi kuendelea kushirikiana na taasisi hiyo kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na magendo ili kulinda uchumi wa nchi na kuimarisha utawala bora.
