Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Mhe. Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya, amesema kuwa taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika huduma za upasuaji wa ubongo kwa kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ya akili unde (Brain Lab) inayosaidia kuongeza usahihi wakati wa upasuaji.
Akizungumza katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Machi 2,2026, jijini Dodoma, amesema kuwa MOI inahudumia takribani wagonjwa laki moja na elfu themanini, ambapo kati yao wagonjwa elfu kumi wamepewa huduma za kibobezi ikiwemo upasuaji.
Pia,Amesema kuwa kupitia teknolojia hiyo, wataalamu wa MOI sasa wanafanya upasuaji wa ubongo kwa uhakika zaidi tofauti na ilivyokuwa awali ambapo walitegemea zaidi makadirio ya picha za vipimo kama CT Scan.
Aidha amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi kumi na mbili iliyopita, taasisi imeanzisha huduma tisa mpya zikiwemo za upasuaji wa ubongo kwa kutumia akili unde, jambo lililoongeza ufanisi na kupunguza madhara kwa wagonjwa.
Amesema kuwa matumizi ya akili unde yanamwezesha daktari kutambua kwa usahihi eneo lenye tatizo ndani ya ubongo na kufanya upasuaji kwa umakini mkubwa bila kuathiri sehemu zisizo na ugonjwa.
Pia ameongeza kuwa sambamba na matumizi ya akili unde, taasisi imeanza kutumia wino maalum unaoitwa Floris Cain pamoja na miwani maalum inayomsaidia daktari kuona mipaka halisi ya uvimbe wakati wa upasuaji.
Amesema kuwa teknolojia hiyo imeongeza kiwango cha mafanikio katika kuondoa uvimbe wa ubongo, kwani sasa daktari anajua ugonjwa unakoma mahali gani na kuondolewa kikamilifu bila kuharibu sehemu nyingine za ubongo.
Aidha amebainisha kuwa MOI inahudumia takribani wagonjwa laki moja na elfu themanini kwa mwaka, ambapo kati yao wagonjwa elfu kumi hupata huduma za kibobezi ikiwemo upasuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu.
Mhe. Balozi Dkt. Mpoki , ameongeza kuwa kuanzishwa kwa akili unde ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za kibingwa nchini, na kwamba taasisi itaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia hiyo ili kuwahudumia wagonjwa kwa viwango vya kimataifa.





