NA FAUZIA MUSSA
KAMPUNI ya mawasiliano ya Halotel Tanzania kupitia tawi lake la Zanzibar imetoa hundi ya shilingi milioni 10 kwa Taasisi ya Majlis Al Maarifa Islamiya kwa ajili ya kutekeleza mpango wa uzalishaji wa vifaa vya usalama barabarani.
Makabidhiano hayo yalifanyika katika ofisi za kampuni hiyo Maisara, Mjini Unguja, ambapo Ofisa kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Sajenti Staff (SSGT) Ali Abdalla Juma, alisema msaada huo ni ishara ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Alisema takwimu za ajali zinaonesha bado kuna changamoto, hivyo upatikanaji wa alama na vibango vya tahadhari utasaidia kupunguza hatari, hususan katika maeneo yenye msongamano wa watu.
“Vibango na vizibao vya usalama vinamkumbusha dereva kupunguza mwendo na kusimama ili kupisha watembea kwa miguu. Wakati mwingine madereva huendesha wakiwa na msongo wa mawazo, hivyo alama hizi ni kinga muhimu,” alisema Sajenti Ali.
Aliongeza kuwa kupitia hatua hiyo, Halotel imejidhihirisha kama mdau anayeshika hatamu katika kusaidia kampeni za usalama barabarani, huku akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi liko tayari kushirikiana na wadau wengine kuhakikisha ajali zinapungua.
Aidha, aliwataka waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kutii sheria za barabarani na kuwakumbusha watumiaji wote wa barabara kutimiza wajibu wao.
“Endapo kila mmoja atachukua hatua stahiki, ajali nyingi zinaweza kuepukika,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara wa Halotel Tanzania, Abdallah Salum, alisema kampuni hiyo imeamua kuwekeza katika mpango huo kwa kutambua kuwa usalama wa wananchi ni jukumu la pamoja.
“Tunalenga kupunguza ajali na kuokoa maisha ya watumiaji wa barabara.”
Alieleza kuwa vifaa vitakavyozalishwa ni pamoja na alama za barabarani, vibango vya tahadhari na vizibao maalum (safety bibs) kwa mabalozi wa usalama barabarani, vitakavyosaidia kudhibiti mwendo wa magari na kulinda watembea kwa miguu.
“Msaada huu ni sehemu ya mkakati wetu wa uwajibikaji kwa jamii chini ya kauli mbiu ya Better Together. Sisi si kampuni ya mawasiliano pekee, bali ni mshirika wa maendeleo na ustawi wa jamii,” alisema Salum.
Alibainisha kuwa ongezeko la vyombo vya moto limekuwa changamoto katika maeneo ya vivuko vya watembea kwa miguu (zebra crossing), skuli, masoko na viwanja vya michezo, hivyo programu hiyo inalenga kuyawekea mkazo maeneo hayo Unguja na Pemba.
Naye Meneja wa Halotel Tawi la Zanzibar, Aboobakar Adam Ngatomela, alisema mchango huo unadhihirisha dhamira ya kampuni kushiriki kikamilifu katika kulinda maisha ya wananchi.
“Kila mmoja ni mtumiaji wa barabara kwa namna moja au nyingine, hivyo suala la usalama si la kupuuzwa,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Majlis Al Maarifa Islamiya, Sheikh Tahir Khatib Tahir, aliishukuru Halotel kwa kuunga mkono wazo hilo kwa kuchangia asilimia 60 ya gharama za utekelezaji wa mradi huo.
“Tunawahakikishia kuwa fedha hizi zitatumika kama zilivyokusudiwa kwa ajili ya kuzalisha na kusambaza vifaa vya usalama barabarani,” alisema Sheikh Tahir.
Alifafanua kuwa vifaa hivyo vitapelekwa katika maeneo yenye mwingiliano mkubwa wa watu ikiwemo skuli za Mji Mkongwe, Jang’ombe, Kisiwa Ndui, Kiembesamaki, Welezo, Soko la Mwanakwerekwe, Jumbi na maeneo mengine.
Sheikh Tahir aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya barabara, hivyo ni wajibu wa wadau kuhakikisha uwekezaji huo unaendana na kuimarishwa kwa usalama.
“Kwa sasa kuna zaidi ya alama za zebra 600 Unguja na 130 Pemba, na kupitia programu hii zitaboreshwa ili ziwe salama zaidi kwa watumiaji,” alieleza.
Hatua hiyo inaonesha namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na taasisi za kijamii na vyombo vya dola katika kupunguza ajali, kulinda makundi maalum yakiwemo wanafunzi, wazee, watu wenye ulemavu na watalii, na kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria za barabarani nchini.

