Na John Bukuku, Dar es Salaam

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa viwango vya joto la bahari pamoja na mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa vinavyohusishwa na hali ya El Niño, hali inayoweza kuathiri mwenendo wa mvua, upepo na afya za wananchi katika kipindi cha Juni hadi Agosti mwaka 2026.

Akieleza mwelekeo wa hali ya hewa kwa msimu wa Kipupwe (JJA), Mkurugenzi Mtendaji wa TMA amesema joto la bahari katika ukanda wa tropiki ya Bahari ya Pasifiki linatarajiwa kuwa juu ya wastani, jambo linaloashiria kujijenga kwa hali ya El Niño ambayo huathiri mifumo ya hali ya hewa duniani.

Amesema hali hiyo sambamba na ongezeko la joto katika Bahari ya Hindi, hususan upande wa kusini-magharibi mwa bahari hiyo karibu na pwani ya Afrika Mashariki, inaweza kuongeza msukumo wa unyevunyevu kutoka baharini kuelekea nchi kavu na kusababisha vipindi vya mvua zisizo za kawaida katika baadhi ya maeneo ya nchi.

Kwa mujibu wa TMA, msimu wa Kipupwe wa mwaka huu unatarajiwa kutawaliwa na hali ya baridi hadi wastani katika maeneo mengi ya Tanzania, huku maeneo ya nyanda za juu kusini-magharibi, kanda ya kati pamoja na baadhi ya maeneo yenye miinuko yakitarajiwa kushuhudia viwango vya chini vya joto vinavyoweza kufikia nyuzi joto sita Selsiasi.

Aidha, TMA imesema maeneo ya ukanda wa pwani ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi na Mtwara yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani, huku vipindi vya upepo mkali kutoka kusini vikitarajiwa kujitokeza zaidi katika miezi ya Juni na Julai.

Mkurugenzi huyo amesema upepo wa bahari wenye unyevunyevu kutoka mashariki utaongeza hali ya ukungu, mawingu pamoja na mvua za nje ya msimu katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki.

“Pamoja na kuwa msimu wa Kipupwe kwa kawaida huwa wa ukavu katika maeneo mengi ya nchi, mwaka huu kuna uwezekano wa kujitokeza vipindi vya mvua zisizo za kawaida kutokana na mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa inayochangiwa na ongezeko la joto la bahari na hali ya El Niño,” amesema.

Katika tahadhari hiyo, TMA imesema hali ya baridi kali na upepo vinaweza kuongeza magonjwa ya mfumo wa upumuaji ikiwemo mafua, homa ya mapafu pamoja na magonjwa ya macho yanayoweza kusababishwa na vumbi katika maeneo kavu.

Wafugaji wametakiwa kujiandaa na upungufu wa maji na malisho katika baadhi ya maeneo huku wakishauriwa kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti magonjwa ya mifugo, wakati wakulima wakihimizwa kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kilimo kutokana na uwezekano wa mvua za nje ya msimu.

Kwa upande wa sekta za usafiri wa baharini, ujenzi, madini na uchukuzi, TMA imezitaka sekta hizo kufuatilia kwa karibu taarifa za hali ya hewa na tahadhari zinazotolewa mara kwa mara ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na upepo mkali na mabadiliko ya hali ya hewa.

TMA imewahimiza wananchi kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa wa saa 24, siku 10 na mwezi pamoja na tahadhari mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo kwa ajili ya kuongeza usalama na ufanisi wa shughuli zao za kila siku.