Kukamilika kwa barabara ya Kasanga Matai Sumbawanga kutaifanya Bandari ya Kasanga ambayo inahudumia wananchi wa maeneo mbalimbai ya Mwambao wa ziwa Tanganyika wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa na nchi jirani za Zambia, Burundi na Congo DRC kutaimarisha huduma zake kwa kiwango kikubwa na kuongeza mapato ya Mamlaka ya Bandari (TPA) ikiwa ni pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea katika bandari hiyo kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa bandarini hapo Meneja wa Bandari katika ziwa Tanganyika (TPA) Bw. Ajuaye Kheri Msese amesema moja ya changamoto kubwa ya Bandari ya Kasanga ni barabara ya kuingia bandarini hapo ambayo tayari serikali inaendelea kuitengeneza na inaelekea kuimalizia kwa kujenga kiwango cha lami.
“Ikikamilika hii barabara bandari Bandari ya Kasanga itafanya vizuri sana kwa sababu hii ndiyo inayotumika kusafirisha shehena ya Makaa ya mawe kutoka Bandari ya Kiwila Kyela mkoani Mbeya kuletwa hapa na kupakiwa kwenye meli kwenda Burundi na shehena ya Saruji kutoka kiwanda cha Mbeya Cement kwenda nchi za DRC na Zambia”.
Msese ameishukuru serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa usimamizi wa miradi mbalimbali mbalimbali ikiwemo barabara hii, ambayo ni kiunganishi kikubwa kwa Bandari yetu ya Kasanga na maeneo mengine yanayotumia usafiri wa vyombo vya maji kusafirisha mizigo na abiria kupitia hapa.
Ameongeza kuwa sambamba na hilo Mamlaka ya Bandari pia ina mradi wa uboreshaji wa bandari ya Kasanga ambao utatekelezwa na Mkandarasi M/S Shanxi Construction Engeneering Cooperation And Mineral Company ambayo imepatikana mwezi Machi na mkataba umesainiwa Aprili 15/ 2019 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Mradi huu utahusisha upanuzi wa Gati kutoka mita 20 mpaka mita 120 ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia meli 2 kwa wakati mmoja na gharama ya mradi huu ni zaidi ya shilingi bilioni 4.7, mkandarasi alikabidhiwa eneo la ujenzi Aprili 28 mwaka huu na tayari yupo kazini.
Meli ya MV Safina kutoka DRC Congo ikiwa imeegeshwa katika bandari ya Kasanga ikisubiri kupakia shehena ya Makaa ya Mawe na Saruji.
Roli likisubiri kupakua shehena ya Saruji kutoka kiwanda cha Mbeya Cement bandarini hapo.
Shehena ya makaa ya Mawe ikisubiri kupakiwa kwenye meli kuelekea nchini Burundi.
Roli lenye shehena ya Makaa ya mawe likiingia katika bandari ya Kasanga.
Picha mbalimbali zikionyesha mkandarasi wa barabara akiendelea na ujenzi wa barabara inayotoka sumbawanga mpaka bandari ya Kasanga.
Mkandarasi akiendelea na ujeni wa barabara katika kijiji cha Kasanga.
Kazi ya kuweka makaravati inaendelea.