Jeshi la Polisi nchini limeanza uchunguzi kufuatia kusambaa kwa picha mjengeo kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha wanawake wawili wakimpiga mwanamke mmoja kwa kutumia mwiko huku wakimshambulia kwa maneno.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, tukio hilo linadaiwa kuhusishwa na madai kuwa mwanamke aliyeshambuliwa alimdhalilisha mmoja wa wanawake hao kupitia mtandao wa Facebook kwa kumtuhumu kuiba waume za watu.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi yeyote mwenye taarifa au anayewafahamu wanawake wanaoonekana kwenye picha hiyo kuwasilisha taarifa katika vyombo vya dola au kwa njia yoyote iliyo rahisi ili kusaidia kuwabaini na kuwakamata wahusika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.




