Mkurugenzi Mkuu Dkt. Adam Fimbo akifungua kikao cha Baraza la Sita la Wafanyakazi

Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Adam Fimbo akifungua Baraza la Sita la Wafanyakazi
………….
Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, ametoa pongezi kwa wajumbe wa Baraza la Sita la Wafanyakazi wa TMDA kufuatia muda wao wa kuhudumu kufikia kikomo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao cha mwisho cha Baraza hilo kilichofanyika tarehe 5 Februari 2026 mkoani Morogoro, Dkt. Fimbo amesema Baraza la Sita la Wafanyakazi lililodumu kwa miaka mitano limekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya TMDA. Amesema mafanikio hayo yametokana na mahusiano mazuri baina ya uongozi na wafanyakazi kupitia ushirikishwaji wao katika maamuzi makubwa yenye kuleta tija kwa taasisi, hususan kupitia vikao mbalimbali vya Baraza.
Dkt. Fimbo amesema katika kipindi cha Baraza hilo, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kukamilika kwa jengo la Ofisi ya Makao Makuu ya TMDA jijini Dodoma, ujenzi wa nyumba za taasisi katika vituo vya mipaka vya Namanga na Tarakea, pamoja na ujenzi wa tanuru la kuteketeza bidhaa duni na bandia kwa lengo la kulinda afya ya jamii.
Aidha, ameongeza kuwa Baraza hilo limehusika pia katika mafanikio ya TMDA kufikia ngazi ya 3 ya ukomavu wa Shirika la Afya Duniani (WHO ML3) na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufikia hadhi hiyo. Vilevile, maabara ya TMDA imetambuliwa na WHO kuwa miongoni mwa maabara bora duniani, huku taasisi hiyo ikiteuliwa kuwa Kituo cha Umahiri cha udhibiti wa dawa, chanjo na utoaji wa mafunzo ya kiudhibiti barani Afrika.
Pia, Baraza hilo limechangia katika kuweka mazingira mazuri ya uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya dawa za binadamu 19, dawa za mifugo 2 na vifaa tiba 41 nchini, amesema Dkt. Fimbo.
Naye Mwakilishi wa Ofisi ya TUGHE Makao Makuu, Wkl. Mwanaidi Mgowa, amepongeza uongozi wa TMDA kwa kuwa na Baraza la Wafanyakazi la mfano wa kuigwa na mabaraza mengine. Aidha, ametoa wito kwa wajumbe wa TUGHE kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa ngazi ya Mkoa na Taifa utakaofanyika ndani ya mwaka 2026.
Akitoa salamu za Kamishna wa Kazi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Bw. Peter Sembuyagi amepongeza uongozi wa TMDA kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia dhana ya ushirikishwaji, ambayo ni takwa la kisheria mahala pa kazi.
Baraza la Wafanyakazi la TMDA hudumu kwa kipindi cha miaka mitano na linaundwa na Menejimenti, wajumbe wa TUGHE pamoja na wawakilishi kutoka ofisi zote za kanda. Baraza hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili masuala makubwa ya kitaasisi ikiwa ni njia mojawapo ya kuwashirikisha watumishi katika ngazi za maamuzi.

Wakili Mwanaidi Mgowa kutoka Ofisi ya TUGHE Makao Makuu akieleza jambo..

Sehemu ya Wajumbe wa Baraza wakijadili jambo katika kikao cha Baraza





