Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Umoja wa Ulaya kufuatia mafanikio ya ziara ya mashauriano ya ngazi ya juu yaliyofanyika jijini Brussels, Ubelgiji. Ziara hiyo iliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Thabit Kombo.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri Kombo alifanya mazungumzo na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya wakiwemo Makamu wa Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya na Mwakilishi Mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje na Usalama, Mheshimiwa Kaja Kallas; Kamati ya Kisiasa na Usalama (PSC); Makamu wa Rais wa Bunge la Ulaya, Mheshimiwa Younous Omarjee; pamoja na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Jozef Síkela.
Ushirikiano huu unaakisi mwelekeo wa diplomasia ya Tanzania yenye kujiamini, inayozingatia maslahi ya taifa, maendeleo, ushirikiano unaolenga matokeo na utekelezaji wa vitendo wa makubaliano ya kimataifa.
Akiambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri Kombo alifanya mashauriano ya kina na Mheshimiwa Kaja Kallas yaliyolenga kuimarisha ushirikiano wa vitendo kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya. Maeneo yaliyosisitizwa ni pamoja na amani na usalama wa kikanda, biashara inayozingatia utawala wa sheria, uwezeshaji wa uwekezaji, pamoja na mifumo thabiti na inayotabirika ya utekelezaji wa miradi.
Ziara hiyo pia ilijumuisha mashauriano na Kamati ya Kisiasa na Usalama (PSC) katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya. Kamati hiyo, inayoundwa na Mabalozi wa Nchi Wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya, ndiyo chombo kikuu cha kuunda na kusimamia sera za mambo ya nje, usalama na ulinzi wa Umoja huo.
Katika kikao hicho, Mheshimiwa Waziri Kombo alisisitiza umuhimu mkubwa ambao Tanzania inaipa taasisi hiyo ya kimkakati, akieleza mitazamo ya Tanzania ndani ya mifumo ya maamuzi ya Umoja wa Ulaya na kuthibitisha nafasi ya Tanzania kama mshirika wa kuaminika katika masuala ya amani, usalama na utulivu wa kikanda katika Afrika Mashariki.
Katika ngazi ya kibunge, Waziri Kombo alifanya mazungumzo katika Bunge la Ulaya, ikiwemo mikutano na Makamu wa Rais wa Bunge hilo, Mheshimiwa Younous Omarjee. Mazungumzo hayo yaliimarisha diplomasia ya kibunge kama nguzo muhimu ya uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, hususan katika biashara, utawala bora na mahusiano ya watu kwa watu.
Masuala ya ushirikiano wa maendeleo na uhamasishaji wa uwekezaji yalikuwa ajenda kuu katika mazungumzo na Kamishna Jozef Síkela. Tanzania ilisisitiza kipaumbele cha ushirikiano unaojikita katika miradi inayotekelezeka na yenye athari chanya, ikilenga ajira, maendeleo ya ujuzi, uongezaji thamani na miundombinu imara, sambamba na Ajenda ya Taifa ya Mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii.
Mashauriano ya Brussels yanaendana kikamilifu na mwelekeo wa sera ya mambo ya nje ya Tanzania uliobainishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Katika hotuba yake ya Mwaka Mpya kwa mabalozi, Rais Samia alisisitiza diplomasia inayojengwa juu ya uhalisia, heshima kwa mamlaka ya taifa, na mawasiliano endelevu na washirika wote.
Kiini cha sera hiyo ni heshima ya pande zote, usawa na manufaa ya pamoja, huku Tanzania ikiendelea kujenga mifumo ya ushirikiano inayochochea maendeleo ya taifa na kutoa thamani kwa washirika wa kimataifa.
Mashauriano haya pia yanaendana na vipaumbele vya ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya vinavyojikita katika maendeleo ya kijani, maendeleo ya rasilimali watu, ajira na utawala bora, na hivyo kuimarisha utekelezaji wa programu na uhamasishaji wa uwekezaji.
Kama sehemu ya diplomasia ya umma, Mheshimiwa Waziri Kombo alifanya mahojiano na jarida la Diplomatic World katika Ubalozi wa Tanzania mjini Brussels, akieleza kuwa ziara hiyo ni uwekezaji wa makusudi katika kujenga imani, kupanua fursa za ushirikiano na kuimarisha taswira ya Tanzania kama taifa thabiti, linaloaminika na lenye fursa za biashara na uwekezaji.
Ushirikiano na Umoja wa Ulaya unaendelea kuwa wa umuhimu mkubwa hususan katika kipindi baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025. Tanzania imeendelea kushirikiana kwa uwazi na mtazamo chanya na Umoja wa Ulaya, ikiwemo katika utekelezaji wa taratibu za kitaasisi kama kazi ya Tume Huru ya Uchunguzi kuhusu matukio ya baada ya uchaguzi.
Mazungumzo endelevu yanawezesha michakato ya kitaifa kueleweka vyema huku yakilinda mwendelezo wa ushirikiano wa maendeleo, mtiririko wa uwekezaji na imani ya kiuchumi.
Ujumbe wa Tanzania ulioongozwa na Mheshimiwa Waziri Kombo ulijumuisha Mheshimiwa Profesa Palamagamba Kabudi, Balozi Swahiba Mndeme, Balozi Jestas Abuok Nyamanga pamoja na maafisa wengine waandamizi.
Ujumbe huu wa ngazi ya juu unathibitisha kuwa Tanzania si mpokeaji tu wa ushirikiano wa kimataifa, bali ni mshirika hai, mwenye kujiamini na anayechagiza mahusiano yake ya kimataifa kwa manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

