NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amezitaka halmashauri zote mkoani humo kuhakikisha zinatoa na kutumia ipasavyo fedha zilizotengwa kwa ajili ya afua za lishe, ili kuimarisha mapambano dhidi ya udumavu na utapiamlo.
Akizungumza mbele ya washiriki wa kikao cha tathmini ya hali ya lishe katika mkoa huo, Mkuu wa Mkoa aliwapongeza Maafisa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Elimu, Maafisa Utumishi, Maafisa Biashara, Maafisa Habari, na watumishi wengine wa serikali kwa kujitoa kushiriki katika mjadala wa namna ya kuboresha ustawi wa jamii, hasa katika sekta ya lishe.
Amesema licha ya serikali kutambua na kufanya juhudi mbalimbali, bado changamoto ya utapiamlo na udumavu inaendelea kuikabili jamii katika ngazi za familia, vijiji, kata, wilaya na mkoa.
 “Changamoto kubwa kuliko zote ni kuongeza uelewa wa masuala ya lishe katika jamii. Hili ni jukumu la kila mmoja wetu kuanzia ngazi ya familia hadi kwa viongozi wa serikali,” alisema.
Akimnukuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mkuu huyo wa Mkoa alisema mkataba wa utekelezaji wa afua za lishe ulio sainiwa tarehe 30 Oktoba 2022 baina ya Rais na Wakuu wote wa Mikoa umeleta msukumo mkubwa katika usimamizi wa suala hilo nchini.
Katika Mkoa wa Iringa, mkataba huo ulisainiwa rasmi tarehe 24 Oktoba 2022 kati ya Mkuu wa Mkoa na Wakuu wa Wilaya, kisha wakurugenzi na watendaji katika ngazi mbalimbali.
Amesema hatua hiyo imelenga kuweka uwajibikaji wa pamoja na kuhakikisha kila ngazi ya jamii inapimika kwa vigezo vinavyokubalika kitaifa.
Mkuu wa Mkoa alibainisha kuwa viashiria vyote 13 vya mkataba wa lishe vinatekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha, hatua aliyosema inachangiwa na usimamizi mzuri na uwajibikaji wa watendaji.
Hata hivyo, alieleza kuwa changamoto kubwa iliyobaki ni matumizi ya fedha za lishe, ambapo hadi kufikia Desemba 2025 halmashauri nyingi hazijatenga wala kutumia fedha kwa mujibu wa mipango.
“Halmashauri ya Mji wa Mafinga pekee ndiyo imetumia fedha zote kama ilivyopangwa. Manispaa ya Iringa na Halmashauri ya Kilolo zimetumia asilimia 39 pekee. Hii siyo sawa.”
Katika hotuba yake, Mkuu wa Mkoa alitoa maagizo matatu makuu kwa halmashauri zote ambapo alisema jambo la kwanza ni Kutoa fedha zote za lishe kwa wakati na kuhakikisha zinalipwa kwa kutumia mifumo sahihi ya kifedha.
Kheri alisema kuwa suala la Idara ya Manunuzi kuhakikisha manunuzi yote yanaonekana kwenye mfumo ili kuepuka taarifa zisizosomeka.
Aliongeza kuwa Idara ya Mipango kusimamia matumizi sahihi ya fedha na kuzuia kuingizwa kwa shughuli zisizo za lishe kwenye bajeti ya lishe.
Alionya kuwa baadhi ya halmashauri zimekuwa zikichanganya bajeti kwa kugharamia miradi isiyo ya lishe kwa fedha hizo, jambo ambalo ni kinyume cha mkataba na mwongozo wa serikali.