Waziri wa Katiba na Sheria ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Dkt Juma Zuber Homera,akigawa Madaftari na sare za shule kwa mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Lusewa Klishima Athumani alipokuwa akizindua mpango wa kugawa vifaa vya shule kwa wanafunzi wanaoishi kwenye mazingira magumu katika Jimboni humo.
……….
Na Muhidin Amri, Namtumbo
WAZIRI wa Katiba na Sheria Dkt Juma Homera,ameendelea kugusa mioyo ya wananchi wenye uhitaji baada ya kutoa msaada wa Madaftari 3,000 na sale za shule 3,000 kwa wanafunzi wanaoishi na kutoka kwenye mazingira magumu katika Wilaya ya Namtumbo.
Akizungumza baada ya kukabidhi Madaftari na sare hizo Dkt Homera alisema,dhamira yake ni kuendelea kutoa vifaa vya shule kwa watoto kwa ajili ya kuwaongezea hamasa ya kupenda kusoma na kuendelea na masomo ili waweze kutumiza ndoto zao.
Alisema,msaada huo ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta ya elimu hapa nchini.
Kwa mujibu wa Dkt Homera ni kwamba,ameamua kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuwa hawana uwezo wa kununua vifaa mbalimbali vya shule,hivyo msaada wake amepeleka kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na wale wanaotoka kwenye mazingira magumu ili waweze kupata elimu kama wanafunzi wengine.
Amewaomba wadau mbalimbali Wilayani Namtumbo na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla,kutoa kipaumbele katika sekta ya elimu kwa kutoa misaada hasa kwa watoto yatima na wenye mazingira magumu ambao wanaweza kukatisha masomo na kupoteza ndoto zao kutokana na kukosa mahitaji yao.
Amewaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na Sekondari Wilayani humo,kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayerudishwa nyumbani wala kukataa kupokea wanafunzia ambao hawana sare za shule badala yake wawapokee wakati wazazi wao wakiendelea kutafuta fedha za kuwanunulia vifaa.
Waziri Homera alisema, kwa kuwa Serikali inatoa elimu bure hivyo watoto wote walioandishwa kuanza shule ya awali,msingi na kidato cha kwanza katika Wilaya ya Namtumbo wanapaswa kuhudhuria masomo licha ya kutokuwa na sare ambapo amewataka wazazi na walezi kupeleka watoto wao ili kupata elimu.
“Daftari hizi pamoja na sale za nimenunua kwa fedha zangu kwani nimeona kuna haja ya kuwasaidia watoto wanaopenda kusoma lakini hawana mahitaji muhimu,nawaomba watu wengine kujitokeza kusaidia makundi mengine yenye uhitaji yaliyopo katika jamii yetu”alisema Dkt Homera.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Namtumbo Zuber Lihuwi,amewasisitiza wazazi Wilayani humo kuhakikisha wanapeleka watoto wao shule na kuacha tabia ya kuwarithisha kazi za nyumbani ikiwemo kilimo na kuchunga mifugo.
Alisema,licha ya Serikali kutoa elimu bila malipo,lakini bado baadhi ya wanafunzi wanakabiliwa na changamoto ya kukosa madaftari,sare,viatu na mabegi kutokana na kipato duni cha wazazi na walezi wao na kumpongeza Dkt Homera kwa moyo wake wa huruma kwa jamii.
Wakizungumza baada ya kupokea msaada huo baadhi ya wanafunzi walionufaika na msaada huo Juma Ramadhan na Binaiza Hosai wa shule ya msingi Lusenti,wamemshukuru Waziri Homera kwa msaada huo kwani utawasaidia kupenda shule,kusoma kwa bidii na kupunguza tatizo sugu la utoro miongoni mwao.
Juma Ramadhan mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Lusenti alisema,ndoto zake za kuendelea na masomo zilianza kufifia kutokana na changamoto za maisha ya wazazi wake kwani alijisikia vibaya kwenda shule akiwa amevaa nguo za nyumbani huku wenzake wamevaa sare za shule.
Binaiza Hosai,licha ya kumshukuru Mbunge Homera kwa msaada huo,hata hivyo ameiomba Serikali kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zenye maisha magumu.
