NA DENIS MLOWE ,IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, ameiongoza jamii ya Mkoa wa Iringa kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Iringa Girls.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa alisema wananchi wa Iringa wamejumuika kuonesha upendo na kutambua mchango wa Rais Samia katika kulinda na kuhifadhi mazingira, akisisitiza kuwa kiongozi huyo ni mpenzi na mtetezi wa mazingira nchini.
“Sisi wanaIringa tunafahamu kwamba Mheshimiwa Rais ni mtu anayeamini katika uhifadhi wa mazingira hivyo tumeungana kupanda miti ili kuunga mkono juhudi zake na kuhakikisha tunalinda ardhi na rasilimali za nchi yetu,” alisema Kheri James.
Katika zoezi hilo, aina mbalimbali za miti zilipandwa zikiwemo miti ya matunda, miti ya kivuli, miti ya dawa na miti inayosaidia kuzuia mmomonyoko wa ardhi, hatua inayolenga kuimarisha mazingira na kuleta urithi bora kwa vizazi vijavyo.
Akiendelea kuhutubia, Mkuu wa Mkoa alisema wamechagua kufanya tukio hilo katika Shule ya Wasichana Iringa Girls kwa makusudi, ili kuwaonesha wanafunzi kuwa wao ni sehemu muhimu ya viongozi wa kesho, hususan wanawake watakaoendelea kulijenga taifa.
“Tumekuja hapa kwa sababu tunaye Rais mwanamama na hapa tunawaandaa marais na viongozi wanawake wa kesho,” alisema.
Aliwapongeza walimu, wanafunzi na watumishi wa shule hiyo kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo, akiwataka kuwa mabalozi wa utunzaji mazingira katika jamii zao.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wanafunzi, pamoja na wadau wa mazingira, ambao walipata nafasi ya kutoa salamu maalum za kumtakia Rais Samia maisha marefu na mafanikio katika kuongoza taifa.
Kwa upande wake Lulu Hamidu Ngatumbura, Mkuu wa Shule ya Sekondari Iringa, ameeleza kuwa leo shule imejumuika kwa furaha kubwa baada ya kupata bahati ya kutembelewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mheshimiwa Kheri James, aliyeungana nao katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkuu huyo wa shule alisisitiza kuwa wanaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais katika uhifadhi wa mazingira, na kwamba wanafunzi wa kike na wa kiume wanayafurahia matunda ya Serikali kupitia mazingira bora ya kujifunzia.
Ameeleza kuwa shule ina majengo ya kutosha, vitabu vya kutosha, walimu wa kutosha, na huduma zote za msingi zinazotolewa kupitia Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aliongeza kuwa kwa siku ya leo, wanafunzi na walimu wamefurahi kwa dhati kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa kiongozi huyo huku wakitambua mchango wake mkubwa katika kuboresha elimu nchini. Amehitimisha kwa kumpongeza tena Mheshimiwa Rais na kueleza kuwa ni mdau mkubwa wa mazingira.
Baadhi ya wanafunzi wakiongea kwa niaba ya wenzao wametoa salamu za pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa. Wameeleza upendo na shukrani zao kwa uongozi wake imara, busara na mchango mkubwa katika kuimarisha elimu nchini.
Mariamu Edward (Kidato cha Sita – HGL) amempongeza Rais Samia kwa kuwa kiongozi mahiri na mstari wa mbele katika utunzaji wa mazingira, hususan kwa utamaduni wake wa kupanda miti kila siku ya kuzaliwa.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya manispaa Iringa Zainabu Mlawa amesisitiza kuwa Rais Samia ni mfano wa mwanamke jasiri anayewawezesha wanafunzi wa kike kujiamini na kutia nia ya kuwa viongozi wa baadaye.
Ametoa shukrani kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika shule hiyo ikiwemo ujenzi wa madarasa, mabweni na viwanja vya michezo, jambo lililoboresha mazingira ya kujifunza.
Amesema kwa ujumla wamemtakia Mheshimiwa Rais maisha marefu, afya njema na uongozi wenye mafanikio, wakisisitiza kuwa wanaendelea kumpenda na kumheshimu.
Aliongeza kuwa wamefanikiwa kupanda miti zaidi ya 587 ambayo imepandwa katika shule mbalimbali mkoani hapa .

