Na Miza Kona Maelezo Zanzibar 27/01/2026
Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohamed Mwalim Simai ameitaka jamii kujua na umuhimu wa vipimo ili kupata huduma za bidhaa zilizosahihi na zenye uhakika kwa wafanyabiashara.
Ameyasema hayo Mikunguni Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, wakati akitoa elimu juu ya umuhimu wa vipimo kwa wanafunzi wa skuli ya Ufundi Mikunguni amesema vipimo vinasaidia kukinda usalama wa bidhaa na mfanyabiashara hivyo kuna umuhimu wa kutolewa elimu ya utumiaji wa vipimo kwa jamii ili kujua vipimo sahihi kwenye mizani kwa wafanyabiashara.
Amesema Wakala wa Vipimo inafanya ukaguzi katika maeneo yote ya Unguja na Pemba ili kuona usawa unafanyika kati ya muuzaji na mfanyabiashara wakati wa kufanya vipimo pale wanapopima bidhaa kwa kutumia vyema mizani zao ili kumlinda mtumiaji na mzalishaji
“Wakala imekuwa ikifanya ukaguzi kwa wafanyabiashara kutambua aina ya mizani zinazotumiwa na wafanyabiashara kwani tayari wamepatiwa maelekezo juu ya mizani zinazotakiwa kutumika kwa uuzaji wa bidhaa ili kuondosha udanganyifu kwa wafanyabiashara” ameeleza Mkurugenzi huyo.
Amefahamisha kuwa zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa sheria namba 6 ya mwaka 2020 inayomtaka wakala wa vipimo kufanya ukaguzi kwa mizani zinazotumiwa na kuhakikisha anatoa majibu sahihi kupitia mizani katika miamala ya biashara kwa wafanyabiashara.
Aidha ameeleza kuwa lengo la kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi ni kueneza elimu ya umuhimu wa vipimo kwa jamii ili kuona kila mmoja anapata elimu hiyo kwa maslahi ya taifa.
Mwalimu wa somo la uhadisi skuli ya Mikunguni Mhandishi Laylat Nassor Issa amesema kutolewa kwa elimu hiyo ni kuongeza chachu kwa wanafunzi kwenye kutumia mitaala mipya ya elimu inayosomeshwa na wataalamu na walimu kwa nadharia na vitendo na kuongeza ubunifu kwa wanafunzi.
Aidha amewataka walimu kuufanyia kazi mtaala mpya unaofundishwa kwa kuzingatia njia za vitendo kwenye utumiaji mizani kujua aina ya mizani inayotakiwa kutumiwa na wafanyabiashara.
Kwa upande wao wanafunzi wa skuli hiyo waliishukuru serikali kupitia Wakala wa Vipimo kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi na kueleza kuwa elimu hiyo wataifikisha kwa jamii na kuahidi kutumia vyema elimu hiyo kwenye masomo yao hasa somo la hisabati kwani kujua tathmini ya somo hilo pale wanaposoma kwa vitendo.
Aidha aliawataka wanafunzi kutokubali kuuziwa bidhaa kwa kutumia mizani ambazo hazina sifa ya kupimia bidhaa na kusisitiza kuelimisha jamii kutambua aina za mizani zinazotakiwa kutumiwa na wafanyabiashara ili kila mmoja ajue umuhimu wa vipimo na kuepuka kudhulumiwa.

