Na Silivia Amandius.
Bukoba, Kagera.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Kagera umeungana na wananchi kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kufanya zoezi la upandaji miti 2,000 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Omumwani, iliyopo Manispaa ya Bukoba.
Zoezi hilo limeongozwa na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kagera, Faris Buruhani, likiwashirikisha wanafunzi wapatao 650 wa shule hiyo, walimu pamoja na vijana kutoka kata mbalimbali za Manispaa ya Bukoba. Mbali na kupanda miti, washiriki walikata keki na kuimba nyimbo mbalimbali za kumtakia Rais Samia maisha marefu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Faris Buruhani amesema vijana wa mkoa wa Kagera wanaendelea kumuunga mkono Rais Samia na kumpongeza kwa uongozi wake uliodumisha amani, mshikamano na utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo inayogusa maisha ya wananchi.
Ameeleza kuwa wameamua kuichagua shule ya wasichana ili kuwatia moyo wanafunzi kuendelea kujituma katika masomo, kutimiza ndoto zao na kuwa viongozi bora wa baadaye. Aidha, amewasisitiza wanafunzi hao kutunza miti iliyopandwa kama sehemu ya kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Omumwani, Juliana Rukweto, ameushukuru uongozi wa UVCCM Kagera kwa kuichagua shule hiyo kuwa sehemu ya maadhimisho hayo, akisema tukio hilo litabaki kuwa kumbukumbu muhimu kwa shule na wanafunzi. Ameahidi kuendelea kuwahamasisha wasichana kusoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao.

