Hanang, 23 Januari 2026
Jimbo la Hanang limepiga hatua kubwa katika uhifadhi wa mazingira baada ya Mbunge wa Hanang, Mh. Asia Halamga, kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) – Hanang, kupanda miche 350 ya miti ya matunda na kivuli katika Shule ya Sekondari Chief Sarja, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mazingira ya kijani na kukuza lishe bora kwa jamii.
Zoezi hilo limewakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali, wanafunzi wa shule hiyo pamoja na wananchi, na kuonyesha mshikamano wa dhati kati ya uongozi wa umma na wananchi katika kulinda mazingira na kuboresha ustawi wa jamii kupitia upandaji miti unaozingatia faida za lishe na kivuli.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mh. Halamga alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira, akieleza kuwa upandaji wa miti ya matunda ni mkakati unaochangia moja kwa moja afya na kipato cha wananchi sambamba na uhifadhi wa mazingira.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Mlima Hanang’ Abubakar Mpapaamesema mpango maalum wa kuendelea kuifanya wilaya hiyo kuwa ya kijani, ikieleza kuwa tarehe 27 Januari 2026 itaadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kupanda miche 1,000 ya miti katika Shule ya Msingi Endaswold na miche 100 katika eneo la Ikulu Ndogo ya Wilaya ya Hanang.
TFS ilieleza kuwa mpango huo unaendana na sera za taifa za uhifadhi wa mazingira na maono ya Rais Samia ya Tanzania ya kijani, yenye rasilimali misitu inayolindwa na kutumiwa kwa tija kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kaulimbiu ya wilaya katika kampeni hiyo imekuwa: “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti.”





