Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha-Rose Migiro, ametoa wito kwa viongozi wa ngazi za juu wa chama, wakiwemo mawaziri, wabunge na madiwani, kushiriki kikamilifu vikao vya mashina na matawi kwa lengo la kubaini changamoto za chama pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Dkt. Migiro ametoa wito huo Januari 20, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, wakati wa mkutano na mabalozi wa nyumba kumi ulioandaliwa kwa lengo la kuimarisha misingi ya chama. Amesema kuwa mashina na matawi ndiyo chemchem ya fikra, ambako mawazo bunifu na mapendekezo ya maendeleo huanzia kabla ya kuwa ajenda za utekelezaji katika ngazi za juu za chama na serikali. Aidha, amebainisha kuwa ushiriki wa viongozi wakuu katika ngazi hizo za chini utaimarisha mshikamano wa chama na kuongeza ufanisi wa utendaji wake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Alhaji Adam Kimbisa, amesema kuwa mabalozi wa nyumba kumi ni nguzo muhimu ya chama, kwani hawachoki wala kunung’unika katika kutekeleza majukumu yao. Ameongeza kuwa mchango wao umeiwezesha CCM kuvuka salama katika kipindi kigumu cha uchaguzi.
Kwa upande wao, baadhi ya mabalozi waliopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo wamesema wanaiomba CCM kuwapatia bima ya afya pamoja na mikopo yenye riba nafuu ili kuwawezesha kujikwamua kiuchumi na kuendelea kulitumikia chama kwa ufanisi zaidi. Mabalozi hao ni pamoja na Paulina John wa Chamwino, Joshua Noha wa Dodoma Mjini na Shaban Said wa Kata ya Ndege.





DKT. MIGIRO AWASISITIZA VIONGOZI CCM KUSHIRIKI VIKAO VYA MASHINA
