Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Media, Dodoma
MADRID, HISPANIA – Klabu ya Real Madrid imeripotiwa kumfuta kazi kocha Xabi Alonso baada ya kushindwa kufikia makubaliano na kuhusu muundo wa benchi lake la ufundi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na gazeti la Marca, uongozi wa Real Madrid ulitaka kufanya mabadiliko katika benchi la ufundi la Xabi Alonso kwa kumjumuisha kocha wa viungo Antonio Pintus. Hata hivyo, Xabi Alonso alikataa pendekezo hilo na kuweka wazi kuwa benchi lake la ufundi ni jambo lisilojadiliwa, akilitaja kama “mstari mwekundu”.
Baada ya pande hizo mbili kushindwa kufikia mwafaka, uongozi wa klabu ulilazimika kuchukua hatua ya kuwafuta kazi Xabi Alonso pamoja na benchi lake lote la ufundi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa maslahi ya klabu, huku mashabiki wengi wakionyesha mshangao kutokana na ukubwa wa jina la Xabi Alonso na matarajio yaliyokuwepo juu yake.
Aidha, Real Madrid tayari imemteua , Mchezaji wa zamani wa klabu hiyo, Álvaro Arbeloa kuchukua nafasi ya Xabi Alonso kama kocha mkuu wa Real Madrid.
Arbeloa amecheza kama beki wa kulia wa Los Blancos na mshindi wa mataji makubwa ikiwemo UEFA Champions League na La Liga, pamoja na mafanikio makubwa ndani ya timu ya taifa ya Hispania.
Baada ya kustaafu, Arbeloa aliteuliwa kuwa kocha wa akademi ya Real Madrid (La Fábrica).



