Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndugu Kenan Kihongosi, leo Januari 12, 2026, amefanya kikao kazi na viongozi pamoja na wasanii wa Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) katika Ofisi Ndogo za CCM, Lumumba.
Kikao hicho kililenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa bendi hiyo, ikiwemo kuimarisha nidhamu, mshikamano na uzalendo miongoni mwa wasanii pamoja na nafasi ya sanaa katika kueneza itikadi, sera na mafanikio ya CCM kwa jamii.
Akizungumza katika kikao hicho, Ndugu Kihongosi aliwasisitiza wasanii wa TOT kutumia vipaji vyao kama chombo cha kuelimisha umma, kudumisha maadili na kuendeleza sanaa yenye tija kwa Taifa, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa weledi na kuilinda heshima ya chama.
Aidha Kenan amewahakikishia viongozi walioshiriki kikao kazi hicho kwamba anatambua kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya kipindi chote cha kampeni za Uchaguzi Mkuu 2025 napia kwa lengo la kukifanya Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuwatumikia wananchi ambao wamekuwa na matumaini makubwa na Chama hicho chini ya Mwenyekiti wao Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande wao, viongozi na wasanii wa Bendi ya TOT walimshukuru Katibu huyo wa NEC kwa kukutana nao na kutoa maelekezo pamoja na ushauri, wakiahidi kuyafanyia kazi ili kuimarisha utendaji wa bendi na kuchangia kikamilifu katika harakati za kijamii na kiutamaduni zinazolenga maendeleo ya Taifa.




