Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, aliyeshika vinasa sauti ,akingumza baada ya kutembelea Hospitali ya Sekou Toure, leo.
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza kimempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita katika miundombinu, vifaa tiba na mashine za kisasa za uchunguzi wa magonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure.
Pongezi hizo zilitolewa na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omar Mtuwa, leo baada ya chama hicho pamoja na jumuiya zake kufanya usafi na kutembelea wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mtuwa alisema CCM imejionea kwa vitendo kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za afya.
“Tumeona mashine ya kisasa ya CT Scan kwa uchunguzi wa magonjwa mbalimbali, mashine za kusafisha damu, mitambo ya kuzalisha hewa tiba (oxygen), vifaa tiba vya kisasa pamoja na jengo jipya la kutolea huduma za afya. Haya ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya CCM,” alisema Mtuwa.
Alisema uwekezaji huo umeongeza ubora wa huduma za matibabu na kuwawezesha wananchi wa Mwanza na mikoa ya jirani kupata huduma kwa urahisi na kwa viwango vya juu.
Aidha, aliushukuru uongozi wa Hospitali ya Sekou Toure kwa usimamizi mzuri wa fedha za miradi ya afya inayotekelezwa na Serikali, pamoja na kuwapongeza madaktari na watoa huduma kwa usafi, nidhamu na ukarimu wanaouonesha kwa wagonjwa.
Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Mwanza, Dotto Omar, alisema ziara yao imelenga pia kujifunza na kushuhudia utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Rais Samia.
“Yaliyofanyika yanatia moyo. Huduma ni bora na zinapatikana kwa wakati. Tumeona mafanikio makubwa hasa katika wodi ya mama na mtoto ambako hakuna changamoto za kimsingi za kitabibu. Tunampongeza Rais Samia kwa kuboresha huduma za afya mkoani Mwanza,” alisema.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Mteja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Daudi Marwa, alisema mafanikio yanayoonekana hospitalini hapo yametokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita.
“Kwa niaba ya uongozi wa hospitali, tunampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa uwekezaji mkubwa uliofanywa hapa Sekou Toure. Jengo kubwa la mama na mtoto pamoja na upatikanaji wa vifaa tiba na mashine za kisasa ni mafanikio ya Awamu ya Sita,” alisema Marwa.
Aliongeza kuwa serikali ina mpango wa kujenga jengo la wagonjwa wa nje lenye ghorofa nane, ambapo fedha tayari zimetengwa na hatua inayofuata ni kubomoa jengo la zamani ili kupisha ujenzi na taratibu za zabuni.
Awali, akizungumza na wafanyabiashara wa samaki katika Soko la Nyamagana, Mtuwa aliwapongeza wananchi kwa kuiunga mkono CCM na kuichagua katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
“Tunashirikiana na wananchi kufanya usafi katika soko hili na tunawashukuru kwa kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi. Serikali inayoongozwa na Dk. Samia imeendelea kufanya kazi kubwa ya kuleta maendeleo,” alisema.
Alisema CCM inatambua changamoto zilizokuwepo awali sokoni hapo na kuipongeza serikali kwa kuwapatia wafanyabiashara eneo bora na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa uhuru katika mazingira salama.
Mwenyekiti wa Soko la Samaki Nyamagana, Raphael Magambo, aliishukuru CCM na Serikali kwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika kudumisha usafi na kuboresha mazingira ya biashara.
Mmoja wa wajasiriamali katika soko hilo, Agnes Samson, alisema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwajengea soko la kisasa lililowaondolea adha ya mvua na jua.
“Hapo awali tulipata shida kwa kunyeshewa mvua na kuchomwa na jua. Sasa tunafanya biashara katika mazingira bora, tunapata kipato, tunasomesha watoto na wengine wameweza kujenga nyumba. Tunamshukuru sana Rais Samia,” alisema.
Baadhi ya Viongozi wa Chama na Jumuiya wakielekea wodi ya wazazi kukabidhi zawadi kwa akinamama waliojifungua.
Mjasiriamali wa soko la samaki, Agnes Samson, leo akiishukuru serikali kwa kuwajengea soko hilo.
Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Mteja wa Hospitali ya Sekou Toure, Daudi Marwa (kushoto), akimweleza Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omar Mtuwa, utekelezaji wa llani hospitalini hapo leo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omar Mtuwa (kulia), akimwaga taka baada ya kufanya usafi katika soko la Samaki Nyamagana, leo.
( Picha na Baltazar Mashaka )



