Na. OWM – TAMISEMI
Hospitali ya Wilaya ya Makete Mkoani Njombe imeongeza idadi ya wagonjwa inaowahudumia kutoka 11,485 mwaka 2021 hadi wagonjwa 26,317 mwaka 2025, ongezeko hilo ni sawa na asilimia 43, hatua inayotajwa kuchochewa kwa kiasi kikubwa na uboreshwaji wa miundombinu na ununuzi wa vifaa tiba uliofanywa na Serikali katika hospitali hiyo.
Hayo yameelezwa leo Januari 8, 2025 na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Halmashauri ya Makete Dkt. Amanda Molel wakati akitoa taarifa juu ya mwenendo wa utekelezaji wa miradi mbalimbali katika hospitali hiyo kwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), anayeshughulikia Afya, Dkt. Jafar Seif aliyefika katika hospitali hiyo kukagua utoaji wa hudma na utekelezaji wa uejenzi wa miradi mbalimbali ya afya katika hospitali hiyo.
Akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo Naibu Waziri Dkt. Seif amewapongeza kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja wao na kuwasisitiza kuendelea kuwahudumia kwa moyo na upendo ili ubora wa miundombinu uende sambamba na ubora wa huduma .
“Tayari Serikali imeboresha Miundombinu, na bado tunaendelea kuleta dawa, na vifaa tiba, kwahiyo kilichobaki ni sisi kama wahudumu wa afya kuwahudumia wateja wetu kwa lugha nzuri, kwa moyo na upendo maana maadili ya kazi yetu ndivyo yanavyotuka, tusiwape wagonjwa msongo wa mawazo bali tuwe msaada kwao” Alisema Naibu Waziri Dkt. Seif.
Hospitali ya Wilaya Makete ni miongoni mwa Hospitali za Wilaya Kongwe ambazo kwa kipindi cha mwaka wa 2020 hadi 2025 zimepokea fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba na ajira za watumishi wa kada mbalimbali za Afya, ambapo kupitia fedha hizo hospitali hiyo imeboresha jengo la huduma za dharua, imejenga uzio kuzunguka eneo lote la Hospitali pamoja na ujenzi wa majengo ya Upasuaji, Maabara, Kufulia, Kichomea taka na ukarabari mkubwa wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD complex).





