Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha Rose Migiro, amesema nguvu halisi ya chama hicho ipo kwa wanachama walioko katika mashina na matawi, akisisitiza kuwa uimara wa CCM haujengwi kwa maelekezo yanayotoka juu bali kwa sauti na maamuzi yanayoanzia ngazi za chini.

Akizungumza mbele ya mamia ya Mabalozi wa Mashina kutoka Wilaya za Temeke na Kigamboni katika kikao kazi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar es Salaam, Dkt. Migiro amesema chama kimefikia hatua ya kuimarisha misingi ya uongozi wa kusikiliza maoni ya wanachama kuanzia mashina, matawi na kata.

Amesema ni wakati wa CCM kuachana na mtindo wa uongozi wa amri kutoka juu kwenda chini, akisisitiza kuwa maelekezo ya kweli ya chama yanapaswa kupatikana kutoka ngazi za chini ambako ndiko wanachama walipo.

“Ninatoa wito kwa viongozi wetu tusifanye utaratibu wa kutoa amri kutoka juu kushuka chini. Uongozi mzuri ni lazima uanzie chini kwenda juu. Yale tunayoyapata kutoka kwenye mashina na matawi ndiyo yatakayopanda juu kwa lengo la kukiimarisha chama chetu,” amesema Dkt. Migiro.

Ameongeza kuwa CCM inapaswa kujenga utamaduni wa kusikiliza wanachama wake walioko chini, akisisitiza kuwa sauti ya mashina ndiyo dira ya uongozi wa chama kuanzia ngazi za kata hadi Taifa.

“Tusikilize kutoka chini kupanda juu, tusiwe chama cha amri zinazoshuka kutoka juu kwenda chini. Hii ni kazi yetu sote—wanachama wa CCM, viongozi wa mashina, matawi, mimi kama Katibu Mkuu na Sekretarieti yote,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Migiro amesema ndani ya Sekretarieti ya CCM wamekubaliana kuwa ziara za chama, hususan za Katibu Mkuu, zianze katika ngazi za chini kwa lengo la kupima umadhubuti na uimara wa chama mahali nguvu ya wanachama ilipo.

“Tumekubaliana kwamba ninapoanza ziara zangu, nianze na mashina, matawi na kata. Ndipo tunapopima uimara wa chama chetu na kujua hali halisi ya wanachama wetu,” amesema.

Ameeleza kuwa azma ya Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kuhakikisha chama kinaendelea kupata uimara unaotokana na mshikamano wa wanachama kuanzia ngazi za chini.

Akiweka msisitizo kwenye suala la itikadi, Dkt. Migiro amesema chama hakiwezi kuwa imara bila kuimarisha elimu ya itikadi, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kurithishwa misingi ya chama kupitia mifumo ya elimu iliyoanzia mashinani.

“Tulijengwa kupitia madarasa ya itikadi kuanzia ngazi za chini kabisa. Tulifundishwa tumetoka wapi, tunaenda wapi, na namna ya kujenga kada ya viongozi waliokita mizizi katika itikadi ya Chama Cha Mapinduzi,” amesema.

Ameongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwatumia wazee na wastaafu wa chama kama hazina ya maarifa na historia ya CCM, ili wawe walimu wa itikadi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

“Tuwatumie wazee hawa kutoa madarasa ya itikadi. Wao wanajua misingi ya chama chetu. Ni hazina muhimu katika kujenga uimara wa Chama Cha Mapinduzi,” amesema.