Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, amesema chama hakina hofu ya kushindwa wala ya kukisemea hadharani, akisisitiza kuwa CCM kina historia ndefu ya mafanikio tangu kuanzishwa kwake, ambayo yameiwezesha Tanzania kufikia hatua ilipo leo.
Kihongosi ameyasema hayo wakati akizungumza katika kikao kazi cha Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM Dkt. Asha Rose Migiro na Mabalozi wa Mashina kutoka Wilaya za Kigamboni na Temeke, kilichofanyika leo kwenye Ukumbi wa PTA Temeke jijini Dar es Salaam.
Amesema historia ya CCM inaonyesha wazi kuwa mafanikio makubwa ya maendeleo yaliyopo nchini leo yametokana na misingi imara ya chama hicho tangu kuasisiwa kwake.
“Naombeni twende tukahubiri amani, upendo na mshikamano kwa Watanzania wote,” amesema Kihongosi.
Ameongeza kuwa viongozi na wanachama wa CCM wanapaswa kwenda kwa wananchi kueleza kwa uwazi utekelezaji wa Ilani ya chama, akibainisha kuwa utekelezaji huo tayari umeanza.
“Twendeni tukawaeleze Watanzania utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na tukahubiri yale tuliyoahidi ndani ya chama chetu,” amesema.
Amesema ndani ya siku 100 za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wa ahadi mbalimbali umeanza kuonekana, ikiwemo hatua za awali za utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.
Aidha, Kihongosi amewataka wanachama na viongozi wa chama kujibu kwa hoja na ujasiri upotoshaji wa aina yoyote, akisisitiza kuwa CCM haitapaswa kubeba au kuruhusu agenda zisizo na maslahi kwa Taifa.
“Tutailinda nchi yetu. Tusikubali kuumiza nchi yetu wala kuruhusu mtu yeyote atuchochee au kuchafua amani ya nchi yetu hapa nyumbani,” amesema.
Amesisitiza kuwa Tanzania si nchi ya majaribio ya watu wanaotaka kuleta vurugu, akiwataka Watanzania wote kulinda amani, mshikamano na heshima ya Taifa.

