Na John Bukuku, Songwe
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limeimarisha ulinzi na usalama kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka 2025 kwa kuongeza doria na misako katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, hatua inayolenga kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuhakikisha wananchi wanaadhimisha sikukuu hizo kwa amani na utulivu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe amesema kuwa doria hizo zinafanywa kwa kutumia magari, pikipiki, askari wa miguu pamoja na Wanyama Kazi (mbwa wa polisi), huku maeneo ya makazi, biashara, barabara kuu na sehemu zenye mikusanyiko ya watu yakipewa kipaumbele maalum.
Katika utekelezaji wa majukumu yake, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limeendelea kupata mafanikio mahakamani baada ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali kuhukumiwa vifungo vya muda mrefu. Kwa mwezi Novemba 2025, watuhumiwa watatu walihukumiwa ambapo Nyati Bugwatu Kapongo (32) alipewa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka, Wailes Tusenche Mwamengo (45) alihukumiwa miaka 20 jela pamoja na faini ya Sh milioni 7 kwa kosa la uhujumu uchumi, huku Yaledi Shadrack Sinkala (38) akihukumiwa kifungo cha miaka 40 jela kwa kosa la kuzini na maharimu.
Polisi pia imeongeza jitihada za kudhibiti usalama barabarani kwa kufanya doria na ukaguzi wa magari katika vizuizi rasmi vilivyopo maeneo ya Senjele na Ihanda. Aidha, vifaa vya kisasa vikiwemo vya kupimia kilevi pamoja na ‘speed radar’ vinaendelea kutumika ili kupunguza ajali zinazotokana na uzembe wa madereva, hususan kipindi cha sikukuu ambacho huambatana na ongezeko la wasafiri.
Sambamba na hilo, wananchi wamehimizwa kuchukua tahadhari wanapotoka majumbani kwenda kwenye ibada, mikesha, sherehe na matamasha, hasa nyakati za usiku, kwa kuhakikisha wanaacha waangalizi kwenye makazi yao. Hatua hiyo inalenga kuzuia wizi na vitendo vingine vya kihalifu vinavyoweza kujitokeza kipindi hicho.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe pia limewakumbusha wazazi na walezi kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto kwa kuhakikisha wanaongozana na watu wazima wanapokwenda ibadani au kushiriki sherehe. Vilevile, wazazi wanahimizwa kuwasaidia watoto kuvuka barabara na kuwaepusha na mazingira au vitendo hatarishi.
Katika kudumisha amani na utulivu, polisi imesisitiza kuwa uchomaji wa matairi sehemu yoyote hauruhusiwi, na yeyote atakayejihusisha na vitendo hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria. Aidha, imepigwa marufuku kwa mtu yeyote kupiga au kulipua fataki bila kibali rasmi, huku waliopata vibali maalum wakitakiwa kuzingatia masharti yote ya usalama.
Kwa upande mwingine, wamiliki wa kumbi za starehe wametakiwa kuhakikisha wanaweka walinzi binafsi katika maeneo ya ndani na nje ya kumbi hizo, hususan maeneo ya maegesho ya magari, ili kuzuia vitendo vya uhalifu. Pia wametakiwa kuzingatia uwezo halisi wa kumbi zao ili kuepuka msongamano unaoweza kusababisha madhara ya kibinadamu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limetoa wito kwa makundi yote ya kijamii kuendelea kuzingatia utii wa sheria bila shuruti na kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati.
Mwisho, Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe limewatakia wananchi wote maandalizi mema ya Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya 2026, likisisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja.




