Na Sabiha Khamis Maelezo 16.12,2025
Jamii imetakiwa kujiunga na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF) ili kuondokana na changamoto zinazojitokeza katika upatikanaji wa huduma bora za afya na kuchangia maendeleo ya taifa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa ZHSF, Khalifa Hilali Muumin, wakati akifungua mkutano wa wanahabari na washawishi ulioandaliwa kwa lengo la kukuza uelewa wa jamii kuhusu mfuko huo. Mkutano huo umefanyika katika Ukumbi wa Sanaa Rahaleo, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema bado kuna changamoto kubwa katika jamii inayotokana na kutokuelewa vyema huduma zinazotolewa na ZHSF, hali inayokwamisha maendeleo ya mfuko huo.
Muumin amebainisha kuwa ndani ya jamii kuna viongozi na watu wenye ushawishi wanaoweza kusaidia kufikisha elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa mfuko huo, hasa ikizingatiwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimarisha sekta ya afya.
Amefafanua kuwa uanzishwaji wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar ni miongoni mwa mipango muhimu ya Serikali yenye lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha. Amesema mfuko huo ulianzishwa ili kukusanya rasilimali fedha zitakazogharamia huduma za matibabu.
“Mfuko huu umeanzishwa kwa lengo la kuwanunulia wananchi huduma za afya ikiwemo dawa, vipimo na huduma nyingine ambazo zimekuwa na changamoto kuzipata kutokana na ukuaji wa taifa letu,” amesema Muumin.
Ameongeza kuwa utaratibu wa matumizi ya mfuko huo bado ni mgeni kwa baadhi ya wananchi, hivyo kuna haja ya kuendelea kutoa elimu ili kuondoa upotoshaji uliopo kuhusu huduma zinazotolewa na ZHSF.
Amesema wanachama wa mfuko huo hunufaika kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wasiokuwa wanachama, ambao mara nyingi hulazimika kutumia gharama kubwa kupata matibabu, hali inayowafanya wengine kuuza mali zao ikiwemo mashamba, nyumba na viwanja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Programu kutoka Shirika la Pharma Access, Faiza Abbas, amesema shirika hilo linaendelea kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha dhamira ya afya bora kwa kila Mzanzibar inafikiwa.
Ameeleza kuwa Serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii, na kusisitiza umuhimu wa wananchi kuchangia ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma hizo.
Ameongeza kuwa washiriki wa mkutano huo wanapaswa kutumia ushawishi walionao katika jamii kufikisha elimu sahihi na kuondoa dhana potofu zilizokuwepo kuhusu Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar.
Naye Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma wa ZHSF, Asha Kassim Biwi, akiwasilisha mada amesema malengo ya mfuko huo ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora na endelevu za afya kwa Wazanzibar pamoja na kupata rasilimali fedha za kugharamia huduma hizo.




