JUMLA ya sh. 407.9 zimetolewa na halmashauri ya wilaya ya Iringa kwa vikundi 71 ikiwa ni asilimia 10 ya mapato ya halmashauri inayotolewa kwa vikundi vya vijana, wanawake na wenye ulemavu.Vikundi 71 vilivyofaidika na mkopp huo vinavyoundwa na wananchi wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na viwanda vidogo katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa.
Mikopo hiyo ya Serikali ina lengo la kuwajengea uwezo wa kiuchumi wananchi na kuongeza ushiriki wao kwenye shughuli za uzalishaji mali hususani vijana, wanawake na wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji wa mikopo hiyo, Saum Kweka, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wilaya ya Iringa amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Serikali la kuhakikisha asilimia 10 ya mapato ya ndani inarejeshwa kwa wananchi kupitia vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Alisema kuwa mikopo hiyo inatarajiwa kuchochea ongezeko la uzalishaji, kukuza ajira na kuinua vipato vya wanufaika katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo hasa yale yaliyopo pembezoni mwa wilaya.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta amesema mikopo hiyo ni Ushahidi wa wazi wa dhamira ya Serikali kushughulika na kero za wananchi
Naye mnufaika wa mikopo hiyo, Dory Sanga aliishukuru serikali kwa kuwainua kupitia mikopo ya asilimia 10 inayowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha na kusema kuwa Mikopo hii kwa kweli imetuinua kwa kiasi kikubwa kwa kuendesha shughuli mbalimbali hususan katika familia zetu kwa kujipatia kipato.





