Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wahitimu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Mwanza wameaswa kuwa waadilifu wanapokwenda kwenye jamii hatua itakayosaidia kutatua changamoto zilipo kwa weledi.
Hayo yamebainishwa Desemba 06, 2025 na Naibu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe.Patrobasi Katambi kwaniaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara Mh.Judithi Kapinga kwenye mahafali ya 60 ya chuo hicho ambapo yanafanyika kwa mara ya 18 katika kampasi ya Mwanza.
Amesema changamoto za kiuchumi,kijamii na kimazingira zipo kila sehemu hivyo wanatakiwa kuwa waadilifu kwa kutumia elimu waliyoipata ili iweze kuleta matokeo yenye tija.
“Nendeni mkatoe mchango wa mawazo kwenye jamii kwani mawazo yenu yanaweza kuleta mabadilko makubwa kwenye maendeleo ya Taifa”.
Aidha, ameeleza kuwa maendeleo hayaji hivi hivi bali Kwa mchakato unaohitaji kujitoa,kujinyima kwa faida ya kesho.
“Kama wahenga wasemavyo mchumia juani hulia kivulini hii inaenda kuthibitisha kwamba katika kipindi chote ambacho mlikuwa katika masomo kitawapelekeeni kufikia kivulini kwa maana ya kuwahudumia watanzania kwakutumia taaluma mliyoipata”, amesema Katambi.
Amesema uaminifu na uzalendo ndio nguzo kuu ya mafanikio hivyo amewaomba wahitimu kuendelea kuwa waaminifu katika kutekeleza majukumu ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kampasi ya Mwanza Profesa Edda Lwoga, amesema jumla ya wahitimu 854 wamehitimu katika ngazi mbalimbali kuanzia Cheti,Astashahada,Stashahada.