Naibu Waziri wa Fedha Mshamu Munde (katikati) akiwatunuku vyeti wahitimu wa ngazi mbalimbali katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampasi ya Mwanza
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Mipango Vijijini (IRDP) wametakiwa kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii kwakutumia elimu waliyoipata hatua itakayosaidia kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Rai hiyo imetolewa leo Ijumaa Desemba 05, 2025 na Naibu Waziri wa Fedha, Mshamu Ally Munde kwaniaba ya Waziri wa Fedha Khamis Omar wakati akizungumza kwenye mahafali ya 39 Duru ya pili ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP) kampasi ya Mwanza yanayofanyika kwa mara ya 13 ambapo jumla ya wahitimu 2,631 wamehitimu katika ngazi mbalimbali kuanzia Cheti, Diploma, Stashahada na Masters.
Amesema kuwa Serikali inawategemea vijana katika kutatua changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa, hasa katika sekta za uchumi na usimamizi wa rasilimali.
Aliahidi kuwa atashirikiana kusimamia ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kikamilifu na kufikia malengo yaliyokusudiwa na Serikali.
Munde aliwataka wahitimu kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya ununuzi, akibainisha kuwa kufanya hivyo kutachangia kukuza uchumi wa nchi na kupunguza tatizo la ajira miongoni mwa vijana.
Vilevile, aliwahimiza vijana kuwa wazalendo katika kulinda nchi, huku akiwataka waendelee kujifunza na kukubali mabadiliko yanayokuja kwa kasi katika ulimwengu wa sasa.
“Ujuzi, nidhamu na kukabiliana na mabadiliko ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya taifa,Serikali itaendelea kuipa chuo ushirikiano ili kuhakikisha kinazalisha wataalam wenye weledi na uwezo wa kujibu mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
Aidha, Naibu Waziri huyo alisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa vyuo kama hivvyo katika Kanda ya Pwani na Kusini, akisema hatua hiyo itawafikia vijana wengi zaidi na kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya kitaaluma.
Aliwasisitiza wahitimu kujiunga na vikundi, jumuiya na mitandao ya kitaalum, akiwataka wajenge mtandao mpana wa marafiki, wadau na wataalam wa maendeleo ambao unaweza kuwasaidia kupata ujuzi, taarifa na fursa za kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini(IRDP), Profesa Hozen Μayaya, amesema kuwa chuo kinaendelea kutekeleza kwa ufanisi miradi mbalimbali ya miundombinu kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Amesema miongoni mwa miradi hiyo ni Miradi iliyokamilika ujenzi wa Maktaba Mpya katika kampasi ya Mwanza, Ujenzi wa Hosteli namba tatu katika Kampasi ya Dodoma.
Profeaa Mayaya amesema miradi hii yote imegharimu zaidi ya shilingi 13, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha miundombinu na kuongeza uwezo wa kuhudumia wanafunzi wengi zaidi.
Amesema miradi inayoendelea kujengwa ni
Ujenzi wa mabweni matano,ujenzi wa ukumbi wa mihadhara wa kisasa,uboreshaji wa matumizi ya Tehama katika ufundishaji na ujifunzaji
Profesa Mayaya amesema kuwa uwekezaji huu unalenga kuongeza ubora wa elimu, kukuza ubunifu na kuzalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa, sambamba na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita kwa kuendelea kuliwezesha chuo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuahidi kuwa IRDP itaendelea kuwa nguzo muhimu katika maendeleo ya rasilimali watu nchini.

Wahitimu Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini Kampasi ya Mwanza wakitunukiwa Astashahada kwenye mahafali ya 39 yanayofanyika kwa mara ya 13




