Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana kwa Ishara Maalum na Mama Mongela katika kutekeleza ushauri wa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kuhusu tahadhari dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona, alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Hyatt Regency Jijini Dar es salaam leo March 04,2020 kwa ajili ya kufungua Kongamano la kuadhimisha na kusherehekea siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 Baada ya mkutano wa beijing.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akisalimiana kwa Ishara na Baadhi ya wajumbe wa Kongamano la Wanawake katika kutekeleza ushauri wa Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kuhusu tahadhari dhidi ya Virusi vya Ugonjwa wa Corona, alipowasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Hyatt Regency Jijini Dar es salaam leo March 04,2020 kwa ajili ya kufungua Kongamano la kuadhimisha na kusherehekea siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 Baada ya mkutano wa beijing.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akifungua Kongamano la kuadhimisha na kusherehekea siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 Baada ya mkutano wa beijing katika Ukumbi wa Mikutano wa Hyatt Regency Jijini Dar es salaam leo March 04,2020. . ambapo kauli mbiu Uwajibikaji wa Uongozi katika kujenga Kizazi cha Usawa wa Jinsia.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akinesha Tuzo aliyokabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa WFT – T Mary Rusimbi kwa kukumbukwa na kutambua mchango wake kwa kusaidia na kuwezesha Wanawake na Watoto pia kwa kuwa kuwa ni Mwanamke wa kwanza Nchini kuweza kushika nafasi ya Juu ya Uongozi wa Makamu wa Rais, baada ya kufungua rasmi Kongamano la kuadhimisha na kusherehekea siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 Baada ya mkutano wa beijing katika Ukumbi wa Mikutano wa Hyatt Regency Jijini Dar es salaam leo March 04,2020. ambapo kauli mbiu Uwajibikaji wa Uongozi katika kujenga Kizazi cha Usawa wa Jinsia. ambapo kauli mbiu Uwajibikaji wa Uongozi katika kujenga Kizazi cha Usawa wa Jinsia.
Mkurugenzi Mtendaji wa WFT – T Mary Rusimbi akimkabidhi Tuzo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kukumbukwa na kutambua mchango wake kwa kusaidia na kuwezesha Wanawake na Watoto pia kwa kuwa kuwa ni Mwanamke wa kwanza Nchini kuweza kushika nafasi ya Juu ya Uongozi wa Makamu wa Rais, Baada ya kufungua rasmimi Kongamano la kuadhimisha na kusherehekea siku ya Wanawake Duniani na Miaka 25 Baada ya mkutano wa beijing
…………………………………………………………………………………
HOTUBA YA MHESHIMIWA SAMIA SULUHU HASSAN,
MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KATIKA KONGAMANO LA KUADHIMISHA NA KUSHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI NA MIAKA 25 BAADA YA MKUTANO WA BEIJING
TAREHE 04 MACHI, 2020 – HYATT REGENCY, DAR ES SALAAM
Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb), Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto;
Mheshimiwa Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam;
Mheshimiwa Sofia Mjema, Mkuu wa Wilaya ya Ilala;
Bi Hodan Addou, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalo husika na Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Mwanamke (UN Women) Tanzania;
Mheshimiwa Paul Sherlock, Balozi wa Ireland nchini Tanzania;
Mheshimiwa Frederic Clavier, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania;
Mheshimiwa Elizabeth Jacobsen, Balozi wa Sweeden nchini Tanzania;
Mheshimiwa pamela O’Donnel, Balozi wa Canada nchini Tanzania;
Wadau wa Maendeleo;
Wawakilishi kutoka Asasi za Kiraia;
Waandishi wa Habari;
Mabibi na Mabwana;
Habari za Asubuhi!
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kujumuika leo hii kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Kwa niaba ya Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninayo furaha kubwa kuungana nanyi kwenye kuadhimisha siku hii. Pili, naomba kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mfuko wa Wanawake Tanzania kwa heshima mliyonipa kuwa Mgeni Rasmi katika kusherehekea siku ya Wanawake Duniani. Maadhimisho ya mwaka huu ni ya kihistoria duniani kote na hapa kwetu Tanzania. Mwaka huu jumuiya ya Kimaifa inakumbuka na kuadhimisha miaka 75 ya kuundwa kwa Umoja wa Mataifa uliotoa tamko kwamba binadamu wote ni sawa.
Aidha, ni mwaka wa 25 tangu mataifa ya umoja huu kutamka mpango kazi wa Beijing uliozitaka nchi wanachama na mashirika yote kuchukua hatua stahiki za kuwezesha upatikanaji wa haki za wanawake na wasichana. Kwa sisi hapa Tanzania ni miaka 20 tangu tuanze kutekeleza Dira yetu ya Taifa yenye kuelekeza kutokomeza aina zote za ubaguzi ikiwemo ubaguzi wa jinsia. Sambamba na hayo pia huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakasababisha kuundwa kwa Serikali na Bunge mihimili ambayo tutaipa dhamana ya kuongoza Dola kwa miaka mitano ijayo kwa turufu ya kura za wananchi wote pamoja na sisi wanawake.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Bila shaka, tuna kila sababu za kujumuika hapa kutafakari kama safari yetu ya kutetea haki za wanawake na wasichana na kupambana na mifumo inayotubagua imefanikiwa. Katika kuitafakari safari hiyo ni vyema tukabainisha mambo gani tumefanya katika nafasi tulizo nazo ili kuleta mabadiliko tunayotamani kuyaona, kumekuweko na fursa zipi, ni changamoto zipi zimejitokeza na tumekabiliana nazo kivipi, na hatimaye, tunataka kuelekea wapi.
Nafahamu kuwa kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya kwa mwaka huu inasema” Kizazi cha usawa kwa maendeleo ya sasa na baadaye”. Kaulimbiu hii imekuja wakati muafaka kabisa ambapo Serikali inaelekeza nguvu kubwa katika kujenga uchumi wa viwanda ili kuleta maendeleo. Serikali inatambua kwamba, tusipochukua hatua za makusudi za kuwekeza kwenye kujenga jamii inayoongozwa na usawa wa jinsia, jitihada zetu za kujenga uchumi wa viwanda na kulikomboa taifa hili kutoka umaskini na kufikia uchumi wa kati haziwezi kufanikiwa.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Sote ni mashuhuda wa jitihada kubwa zilizochukuliwa na serikali katika kutekeleza azma ya kuondoa ubaguzi wa kijinsia na kujenga jamii inayoongozwa na usawa wa jinsia. Katika kuhakikisha hilo, Serikali yetu imeridhiria mikataba yote ya kimataifa na kikanda inayotupa wajibu wa kuchukua hatua za makusudi kuondoa ubaguzi wa jinsia na kuwezesha wanawake na wasichana kupata haki zao bila ubaguzi wa aina yoyote. Tukiwa wanachama wa Umoja wa Mataifa, Serikali yetu ilishiriki kikamilifi katika Mkutano wa Beijing mwaka 1995 (ambao mimi nilibahatika kushiriki nikiwa bado kijana) ulioongozwa na Mama Getrude Mongella. Katika mkutano huo nchi yetu iliridhia Tamko na Mpango Kazi wa Beijing. Mpango Kazi huu ulibainisha maeneo 12 ya kupewa kipaumbele ili kufanikisha juhudi za kuondoa ubaguzi wa kijinsia na kuwezesha wanawake na wasichana kupata haki sawa na wanaume.
Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Mheshimiwa Benjamin Mkapa, ilipokea Mpango Kazi wa Beijing kutoka kwa ujumbe wetu uliokwenda Beijing, kwenye mkutano uliyojulikana kwa jina la “Rudisha Beijing Nyumbani” ikabainisha maeneo kadhaa ya kipaumbele kama vile Wanawake na Umaskini, Ushiriki wa Wanawake katika Meza ya Maamuzi, Elimu na Afya. Aidha Serikali za awamu zote zilibeba na zinaendelea kubeba wajibu wa kutokomeza ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo ubaguzi wa kijinsia. Wajibu huu umehusisha pia kuboresha au kutunga sheria zinazoongoza utekelezwaji wa misingi ya usawa, sera, mipango na mikakati ya kuwezesha taifa kuondoa ubaguzi wa aina yoyote ikiwa ni pamoja na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Katiba zetu zote mbili yaani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na Katiba ya Zanzibar (1984) ambazo ndio sheria mama zinazoongoza sheria zote zinatamka bayana kuhusu usawa wa binadamu na kukataza ubaguzi wa aina yoyote. Katiba hizi pia zinabainisha kuhusu ushiriki wa raia wote Wake kwa Waume kwenye uongozi wa Taifa letu. Mbali ya ushiriki katika uongozi, Katiba hizi zinatamka kuhusu uwepo wa viti maalum vya uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi.
Kazi kubwa iliyofanywa na serikali zetu ni kutafsiri misingi ya vifungu vya katiba na kutunga Sera za kuongoza utekelezaji wa vifungu hivyo. Sera hizo ni kama vile sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ambayo sasa hivi iko kwenye mchakato wa maboresho, sera za elimu, afya, maji na nishati ambazo zote hizo zinalenga kutekeleza azma ya kujenga misingi ya usawa na kuondoa ubaguzi wa kijinsia. Aidha, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, inalenga kuwa na taifa lisilokuwa na aina yoyote ya ubaguzi ifikapo mwaka 2025, ambayo ni miaka miaka mitano ijayo kuanzia sasa. (je itawezekana? ili iwezekane tufanyeje?)
Ili kufanya utekelezaji wa Sera zilizotungwa kuwa na uhalali wa Kisiasa na Kijamii, Sheria mbalimbali zinazobainisha usawa wa jinsia na zinazokataza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake zimetungwa. Kwa mfano, kwa upande wa Tanzania Bara, Sheria za Ardhi za mwaka 1999, Sheria kuhusu Makosa ya Kujamiiana (SOSPA) ya mwaka 1998 na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019. Aidha, Sheria ya Kupambana na Kuzuia Rushwa ya mwaka 2007 inabainisha kuwa rushwa ya ngono ni kosa la jinai linalotokana na matumizi mabaya ya mamlaka, na imebainishwa kuwa ni kitendo cha uhujumu uchumi, kwa kuwa inahujumu rasilimali watu ambao ndiyo wajenzi wa uchumi wa nchi.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Serikali yetu imeweka mikakati na mipango madhubuti ya kuimarisha uchumi na kuondoa ubaguzi wa kijinsia katika nyanja zote muhimu za uchumi. Mipango na mikakati hiyo imelenga kuondoa umasikini na kukuza uchumi kwa upana na ulinganifu (broad-based and inclusive) ili kuwanufaisha wanawake na wanaume, watoto wa kike na wa kiume. Kwa mfano mpango wa kuwezesha wanawake kiuchumi umelenga kifedha na pia kuwajengea uwezo katika shughuli zao za kiuchumi. Kwa sasa halmashauri zote nchini zinatakiwa kwa mujibu wa sheria kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa lengo la kuwakopesha bila riba wanawake (asilimia 4), vijana (asilimia 4) na watu wenye ulemavu (asilimia 2). Ingawa kiasi hicho ni kidogo kulinganisha na mahitaji, lakini tunashuhudia matokeo yenye manufaa kwa wale wanaozipata na kuzifanyia kazi kama walivyokusudia. Maelekezo yangu kwa halmashauri imekuwa ni kupunguza utitiri wa vikundi na kuwapa fedha kidogo na badala yake watoe fedha za kutosha kwa vikundi vichache ili kuweza kupata matokeo chanya na fedha hizo ziweze kurudishwa kwa wakati.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kwa makusudi kugharamikia elimu katika ngazi ya awali, msingi na sekondari. Jitihada hizi zimeongeza idadi ya watoto wanaosajiliwa kujiunga na shule ambapo watoto wa kike wameendelea kuwa wengi kwenye ngazi ya kusajiliwa katika shule za msingi na hata sekondari kwa kidato cha kwanza mpaka cha nne. Sera hii ya elimu bure imemfungulia mtoto wa kike milango ya elimu, ikiwa ni njia sahihi ya kumpa nyenzo za kukabiliana na mifumo kandamzi yenye kumbagua. Changamoto kubwa kwa watoto hawa walioandikishwa ni kuwawezesha kumaliza elimu yao na kufikia ngazi za juu. Kwa upande wa watoto wa kike, mimba za utotoni ni changamoto nyengine kwa baadhi yao kutoweza kutimiza ndoto zao, na lengo la dira ya taifa la kuwa na taifa la wasomi.
Ili kuhakiksha mimba za utotoni zinakoma hatuna budi jamii yote kuwajibika kuanzia kwenye kaya zetu kwa kuondokana na mila na desturi za kumbagua au kutomthamini mtoto wa kike. Katika shule zetu, tuendeleze kumpa nyenzo na shauku mtoto wa kike adhamirie kutimiza ndoto zake. Kwenye ngazi hii, ipo changamoto kwa baadhi ya waalimu wa kiume na wazazi ama walezi kutumia mamlaka yao vibaya na kuwalaghai watoto hatimaye kupata mimba. Serikali inakemea vikali vitendo hivi na itaendelea kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wale wanaofanya vitendo hivyo.
Kwa upande wenu ninyi kama watetezi wa haki za wanawake na watoto, tunatambua kazi kubwa mnayoifanya, na kwa kuwa nanyi mnaishi ndani ya jamii, hamna budi kuwa wepesi wa kuwabainisha wale wanaoendeleza vitendo vya ukiukwaji wa haki na maadili kwa Wanawake na Watoto ili sheria ichukue mkondo wake. Tunahitaji mshikamano wa kitaifa kukomesha vitendo vya kudhalilisha Wanawake na watoto wetu.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Katika kutekeleza agizo la kutoa afya bora kwa kila Mtanzania, kumekuwepo na jitihada nyingi za kupanua huduma za afya ili kumfikia mwananchi wa kawaida hususan huduma za uzazi salama na afya ya mama na mtoto. Jitihada hizi zimeonesha mafanikio kwa kupunguza vifo vya watoto kwa kiasi kikubwa. Changamoto imebaki kwenye vifo vya mama wajawazito ambavyo ni takribani vifo 400 kati ya wamama100,000. Aidha, Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha vifo vya mama wajawazito vinapungua kwa kuendelea kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali za Wilaya na zote zikiwa na wodi maalum kwa ajili ya mama wajawazito na watoto. Hata hivyo, jukumu la usalama wa mama wajawazito haliwezi likaachiwa serikali peke yake. Serikali inaweka miundombinu na wataalam lakini jamii ina jukumu la kuhakikisha akinamama wajawazito wanatunzwa na kujifungulia kwenye vituo vya afya.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Shughuli ya kumtua Mama ndoo kichwani inaendelea vyema, kwa sasa, maeneo mengi yaliyokuwa na shida ya upatikanaji wa Maji yameanza kupata Maji au miradi inaendelea. Kumekuwa na Miradi mikubwa ya Maji maeneo ya Kanda ya Ziwa kwa kutumia Ziwa Victoria na mradi huo unatarajiwa kuhudumia mpaka maeneo ya Tabora na Singida. Mradi wa Same Mwanga na Tanga kwa upande mwa Kaskazini mwa Tanzania, Mradi mkubwa wa maji unaohudumia Dar es Salaam, Kisarawe, Chalinze na Babamoyo (Ruvu Juu na Ruvu Chini), Mradi wa Arusha, Manyara, na maeneo ya Kigoma. Pamoja na miradi hiyo mikubwa, kumekuwa na jitihada za kuchimba visima katika maeneo yasiyo na vyanzo vikubwa vya Maji ili kupunguza uhaba wa rasilimali hio.
Umeme Vijijini ni mradi utakaowanufaisha sana wanawake na kazi hii inaendelea vyema.
Kwenye suala la ushiriki wa wanawake katika meza ya maamuzi, Serikali zetu zimechukua hatua kadhaa ili kuondoa vizingiti vinavyowazuia wanawake wasishiriki kikamilifu katika meza ya maamuzi. Kwa mfano katika mihimili yetu mitatu ya Dola, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uwiano wa kijinsia. Katika Bunge, wanawake ni asilimia 36.7, Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wanawake ni asilimia 38. Katika Mahakama ya Rufani ambayo ni Mahakama ya juu kabisa nchini wanawake ni asilimia 38. Aidha, katika Baraza la Mawaziri la Serikali hii ya Awamu ya Tano wanawake ni asilimia 18 wakati Naibu Mawaziri ni asilimia 33. La kutia moyo zaidi ni kwamba kwa mara ya kwanza katika historia kwa nchi yetu Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanamke. Changamoto ninayoiona kwenye suala hili ni ya uchache wa wanawake wenye uwezo kugombania nafasi mbalimbali iwe kwenye uongozi wa kisiasa, biashara, asasi za kiraia na sekta binafsi. Ni jukumu lenu kama watetezi wa haki za wanawake kushawishi wanawake wenye uwezo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali katika nyaja tofauti.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Ninapokaribia kuhitimisha hotuba yangu mniruhusu kwa mara nyingine nikupongezeni Mfuko wa Wanawake Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya kufanikisha uzinduzi huu. Mimi binafsi na kwa niaba ya Serikali inayoongozwa na jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania naomba niwahakikishie kuwa tutawaunga mkono na tuko tayari kushirikiana nanyi katika shughuli zenu zenye mnasaba wa kumtetea na kumkomboa Mwanamke na Mtoto. Wito wangu kwenu ni kuendelea kushikamana na kutambua kwamba wanawake ni jeshi kubwa katika uchumi, siasa na katika kuleta ustawi wa jamii zetu. Na kwamba tunao uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko tunayoyataka katika kuhakikisha kuwa haki zetu tunazitetea, zinapatikana, na hatimaye tunazilinda.
Mwisho kabisa, napenda tena kuwashukuru waandaji wa shughuli hii kwa kunialika kuja kufanya ufunguzi rasmi wa Kongamano hili. Bila maneno mengi zaidi, sasa natamka kuwa KONGAMANO LA KUADHIMISHA NA KUSHEREHEKEA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI NA MIAKA 25 BAADA YA MKUTANO WA BEIJING limefunguliwa rasmi. Nawatakia majadiliano mema na yenye tija.
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA