Home Mchanganyiko UVCCM SINGIDA YAUNGA MKONO KAMATI KUU KUMNG’OA MEMBE, YATANGAZA KUMCHUKULIA FOMU JPM...

UVCCM SINGIDA YAUNGA MKONO KAMATI KUU KUMNG’OA MEMBE, YATANGAZA KUMCHUKULIA FOMU JPM KUWANIA URAIS KIPINDI CHA PILI

0

Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida, Dkt. Denis Nyiraha akihutubia katika moja ya mikutano ya chama.

 
Na Godwin Myovela, Singida
 
UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida (UVCCM) umefurahishwa na hatua iliyochukuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho ya kumvua uanachama aliyekuwa kada wa chama hicho Bernard Membe, huku ukisisitiza ni mwanzo mpya wa kujenga nidhamu katika muktadha mpana wa ustawi wa chama.
Aidha, pamoja na kurudia mara kwa mara kumpongeza Rais John Magufuli kwa umahiri katika utendaji wake, UVCCM-Singida umejitokeza hadharani na kutangaza kwamba kitamlipia gharama zote, na hatimaye kumchukulia fomu Rais Magufuli ili aweze kuendelea kuliongoza taifa kwa kipindi cha pili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Umoja huo wa Vijana mkoani hapa, Dkt Denis Nyiraha alisema wanaunga mkono na wanabariki maamuzi yote yaliyofanywa na Kamati Kuu kwa kuzingatia kuwa hakuna mwanachama yeyote wa chama hicho aliye juu ya katiba ya chama.
“Membe alikuwa mkaidi, na mara kadhaa amekuwa akivunja kanuni na taratibu za chama waziwazi, tunaomba na wengine wote wenye tabia kama za Membe wasifumbiwe macho, washughulikiwe ipasavyo kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizopo ili kujenga nidhamu ndani ya chama chetu,” alisema Nyiraha.
Aidha, kwa niaba ya UVCCM-Singida, Nyiraha alipongeza serikali ya awamu ya tano kwa namna ilivyojitoa kikamilifu katika kujali maskini na wanyonge, lakini kubwa zaidi kwa namna ya kipekee inavyoibua na kutekeleza miradi mikubwa yenye ustawi na tija kwa maendeleo ya taifa.
“Magufuli ametujengea heshima kubwa ndani na kwenye medani za kimataifa, ni rais wa mfano hakika  tunaona fahari kuwa na kiongozi kama huyu na tunajivunia. Ndio maana kwa moyo mkunjufu na kwa mapenzi ya dhati kwake sisi uvccm-singida tumeamua kumchukulia fomu ili aendelee kufanya makubwa zaidi kwenye kipindi chake cha pili,” alisema Mwenyekiti huyo wa UVCCM.
Nyiraha alisema wanatarajia mapema mwezi Aprili kuwasilisha kwa Katibu Mkuu wa chama hicho taifa Dkt Bashiru Ally malipo ya gharama zote zinazohitajika ili kutimiza azma hiyo.