Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa chama cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara, (MAREMA) Elisha Nelson Mnyawi amewapongeza wachimbaji wa mkoa huo kwa kuendelea na shughuli zao za uchimbaji madini kwa amani bila kusababisha vurugu au uvunjifu wa amani, wakati na baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais uliofanyika Oktoba 29 mwaka huu wa 2025.
Elisha ametoa pongezi hizo kwa wachimbaji hao katika ziara ya Waziri wa Madini Mhe Anthony Mavunde aliyetembelea na kufanya ziara Wilayani Simanjiro, katika machimbo ya madini ya ganeti ya kijani Lemshuku na madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani.
Amesema anawashukuru kwa amani ya kutosha waliyoiendeleza kwani wameonyesha kuwa wachimbaji ni watu wanaojitambua wanaohitaji kufanya kazi zao kwa amani na siyo vinginevyo.
“Niwashukuru sana wachimbaji madini wa mkoa wa Manyara, kwani mmetuonyesha kwamba ninyi ni wachimbaji mnaojali shughuli zenu na kuendeleza amani iliyopo kwani bila amani huwezi kuchimba madini,” amesema Elisha.
Amewapongeza wachimbaji madini wa mkoa huo kwa kuendelea kufanya kazi zao kwa amani bila kujihusisha na vurugu zozote na kujitofautisha na maeneo mengine.
“Wachimbaji wa mkoa wa Manyara nawapongeza sana kwa kuendelea na tabia njema ya kuthamini amani na kutojihusisha na maandamano au vurugu ambazo hazina maana,” amesema Elisha.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo wa MAREMA amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumteua tena Waziri Mavunde kuongoza wizara hiyo ya Madini.
“Tunakupongeza sana kwa uteuzi huu, kwani inaonyesha Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan ana imani kubwa na wewe ndiyo sababu akaendelea kukuamini na kukupa upya dhamana ya kuwa Waziri wa Madini, hongera sana,” amesema Elisha.



