Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa (wa kwanza kushoto) akikagua uharibifu wa miundombinu ya Shule ya Msingi Kisukuru uliyosababishwa na vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, katika ziara ya kikazi aliyofanyika leo Novemba 17, 2025.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa akiwa na uongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Kimanga pamoja na Kaimu Afisa Elimu Kata ya Kimanga Marry Ng’ombo wakiangalia madawati yaliovunjika ya Shule ya Msingi Kisukuru wakati wa vurugu za uchaguzi mkuu.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa akikagua madawati ya Shule ya Msingi Kimanga yaliyonusurika kuchomwa moto wakati wa uchaguzi.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisukuru.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa akizungumza na kamati za Shule ya Msingi Kimanga
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa akizungumza na walimu na kamati za Shule ya Msingi Kisukuru.
……………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala, Comrade Mtiti Jirabi Mbassa, leo Novemba 17, 2025, amefanya ziara ya kikazi katika Shule ya Msingi Kisukuru na Kimanga kwa ajili ya kukagua madhara yaliyosababishwa na vurugu zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Katika ukaguzi huo, Comrade Mbassa ameshuhudia uharibifu mkubwa wa miundombinu ya shule hizo, ikiwemo kuvunjika kwa milango ya madarasa, uharibifu wa madawati, pamoja na kuharibiwa kwa mifumo ya maji na umeme.
Akizungumza na walimu pamoja na kamati za shule za Kisukuru na Kimanga kwa nyakati tofauti, Comrade Mbassa amesema kuwa taarifa ya uharibifu huo itawasilishwa katika idara husika Wilaya ya Ilala ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kurejesha hali ya shule hizo.
“Tutahakikisha taarifa hizi zinafikishwa katika mamlaka husika ili hatua zichukuliwe mapema kadiri inavyowezekana. Ni wajibu wetu kama wazazi na viongozi kulinda mazingira salama ya kujifunzia kwa watoto wetu,” amesema Mbassa.
Aidha, Mbassa amewapongeza walimu kwa kazi kubwa na nzuri wanayoendelea kufanya licha ya changamoto zilizojitokeza, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwalea wanafunzi katika misingi ya nidhamu, uzalendo na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, akibainisha kuwa maadili ni msingi wa kuandaa kizazi bora cha baadaye.
Kwa upande wao, uongozi wa Shule ya Msingi Kisukuru na Kimanga umeishukuru ofisi ya Katibu huyo kwa kufanya ziara hiyo, huku wakisema hatua hiyo imeonesha dhamira njema ya kuhakikisha changamoto zinazozikabili shule hizo zinapatiwa majibu kwa wakati.
Katika ziara hiyo, Katibu Mbassa aliambatana na uongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM Kata ya Kimanga pamoja na Kaimu Afisa Elimu Kata ya Kimanga Marry Ng’ombo ambapo waliahidi kushirikiana na jamii katika kuhakikisha miundombinu ya shule hizo inarejeshwa katika hali yake ya kawaida.




