NA MWANDISHI WETU, LONGIDO
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Kalli, leo Novemba 14, 2025, amemaliza mgogoro wa maji kati ya wananchi wa Kitongoji cha Engasurai kilichopo Kijiji cha Kiserian, Kata ya Engikaret, na uongozi wa Kanisa la Methodist Tanzania ambalo lilijenga kisima kinachotoa huduma ya maji katika eneo hilo.
Mgogoro huo ulitokana na wananchi kutokubaliana na uongozi wa kanisa hilo kuhusu bei ya maji waliyokuwa wakiuziwa ya shilingi 200 kwa ndoo ya maji ya matumizi ya binadamu na mifugo.
Akizungumza na wananchi wa kitongoji hicho, Mhe. Kalli amesema kuwa baada ya mazungumzo baina yake, viongozi wa kijiji na uongozi wa Kanisa la Methodist Tanzania, wamefikia makubaliano mapya ambapo maji yatauzwa shilingi 100 kwa ndoo.
Aidha, kwa upande wa mifugo, kila mnyama atanyweshwa maji kwa gharama ya shilingi 100 bila kujali kiwango cha maji atakachotumia.
“Kisima wenzetu wamekijenga kwa gharama; wanatumia umeme pale, wananunua mafuta ya dizeli. Tunataka kiendelee kuwahudumia ninyi wananchi,” amesema Mhe. Kalli.
Ameeleza kuwa fedha zitakazokusanywa kutokana na mauzo ya maji zitawezesha uendeshaji wa mradi huo, ikiwemo ununuzi wa mafuta ya dizeli yanayotumika kuendesha mashine za kuvuta maji kutoka kisimani hadi kwenye matenki.
Katika wito wake kwa wananchi, Mhe. Kalli amesisitiza umuhimu wa kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo ili kuendelea kudumisha amani katika jamii.
Katika hatua nyingine, amebainisha kuwa Serikali imetenga shilingi milioni 600 kwa ajili ya kuboresha Kisima cha Kijiji cha Kiserian ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Engikaret, Mathayo Ndaiya, amemshukuru Mhe. Kalli kwa kutatua mgogoro huo na kuwataka wananchi kutumia maji hayo kwa uangalifu.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kiserian, Ndete Lengei Laizer, ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanazingatia makubaliano yaliyofikiwa.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kalli ametembelea mnada wa Soko la Kiserian na kusalimiana na wananchi.




