Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi wahimizwa kutumia busara kudumisha utulivu wa taifa
Mwenyekiti wa Taasisi isiyo ya kiserikali Tanzania Jumuishi (TAJU), Ndonge Said Ndonge, amelaani vikali vitendo vya vurugu vinavyosababisha uvunjifu wa amani nchini, hasa vinavyowaathiri watu wenye ulemavu na wengine kupoteza maisha.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ndonge alisema ni wajibu wa kila Mtanzania kulinda amani na utulivu wa taifa, akivitaka vyama vya siasa na viongozi wa dini kutumia nafasi zao kwa hekima na busara ili kuepusha migawanyiko katika jamii.
“Zao la amani ni haki muhimu kwa dunia ya sasa. Ili kulinda amani yetu, hatupaswi kuiga mataifa mengine yanayokumbwa na vurugu zisizo na suluhu. TAJU inawaasa Watanzania kuacha kuiga mambo ya nje yasiyo na manufaa kwa taifa letu,” alisema Ndonge.
Aidha, Ndonge aliwataka wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa njia chanya, akibainisha kuwa si kila taarifa inayochapishwa mtandaoni inafaa kuaminiwa au kuigwa.
Kuhusu suala la uzalendo, Ndonge alisema kila raia anatakiwa kujitathmini katika namna anavyolipenda na kulilinda taifa lake.
“Mzalendo wa kweli si mbinafsi; hutanguliza maslahi ya taifa kabla ya yake binafsi. Tunapaswa kuiga mfano wa viongozi wetu waasisi kama Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Abeid Amani Karume na Edward Moringe Sokoine waliopigania taifa kwa moyo wa uzalendo wa dhati,” aliongeza.
Kwa upande wake, Katibu wa TAJU, Innocent Gabriel Siriwa, aliwasihi Watanzania kufuata taratibu za kisheria wanapokuwa na malalamiko au kutoridhika na jambo fulani, badala ya kuchukua hatua zinazoweza kuleta vurugu au migogoro.
“Tufuate taratibu za kisheria ili maoni yetu yasikike na yafanyiwe kazi. Vurugu hazileti suluhu bali zinadidimiza maendeleo,” alisema Siriwa.
Mwisho, TAJU imeitaka serikali na wananchi kusameheana kwa yote yaliyotokea, ikisisitiza kuwa msamaha ni msingi wa maridhiano na amani ya kweli.
“Popote tulipo, tuendelee kuitunza, kuilinda na kuendeleza amani ya taifa letu la Tanzania,” alihitimisha Ndonge.




