Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaj Hasani Kabeke (wa tatu kutoka kulia walioketi mbele), akiendesha Dua ya kuiombea nchi amani, jijini huumu leo.
Wanaume wa dini ya Kiislamu, wakishiriki Dua ya kuiombea nchi amani.
Wanawake wa Kiislamu, wakishiriki Dua ya kuiombea nchi amani, jijin Mwanza, leo.
Sheikhe wa Wilaya ya Ilemela, Abdulwarith Juma,akieleza umuhimu wa amani.
Mjumbe wa Baraza la Masheikhe Wilaya ya Nyamagana, Ayoub Khatibu,akisisitiza utii kwa viongozi wa dini na serikali.
Sheikhe wa Wilaya ya Misungwi, Hussein Hussein, aliwataka Waislamu kuzingatia maelekezo ya Qur’an badala ya mambo yaliyo nje ya utaratibu.
Shekhe wa Shia Ithna Sheri Kanda ya Ziwa, Sheikhe Hashimu Ramadhan, akieleza kuwa amani hutoka kwa Mungu pia hurejea kwake.
Sheikhe Hasani Kabeke, leo akitaja mambo sita muhimu ya kuzingatiwa ili kutunza amani, baada ya Dua ya kuombea nchi amani.
Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, akiwaongoza waumn wa Dini ya Kiislamu jijini humu, wanaomuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kunyoosha mikono juu, Picha zote na Baltazar Mashaka
………
Na Baltazar Mashaka, Mwanza
Baadhi ya viongozi wa Dini ya Kiislamu mkoani Mwanza wamesema kuwa vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi mkuu ni funzo kubwa kwa Watanzania wote kuhusu thamani ya amani, wajibu wa kuilinda nchi, kudumisha umoja na kuendelea kuwa watiifu kwa mamlaka halali.
Viongozi hao wameyasema hayo leo katika dua maalumu ya kuiombea nchi amani, iliyofanyika katika Msikiti wa Sheikh Abubakary Zuber Bin Ally, jijini Mwanza. Wamesema chanzo kikuu cha machafuko hayo ni ukosefu wa imani, uvumilivu na heshima kwa mamlaka, mambo ambayo yamekuwa yakihatarisha mshikamano wa kitaifa.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaj Hasani Kabeke, amesema vurugu hizo zimetokana na watu walio nje ya nchi kuwajaza vijana sumu ya chuki, hali iliyochochea vurugu na kuhatarisha utulivu wa Taifa.
Akitaja mambo sita muhimu ya kuzingatia ili kudumisha amani ambayo ni kuhifadhi nafsi, kulinda mali, dini, heshima au cheo cha mtu, uadilifu na nchi, Sheikh Kabeke amesema kuwa mambo hayo yote yanafanyika pale ambapo kuna amani.
“Haki hupatikana pale tu panapokuwepo amani. Tulichoona siku tatu zilizopita ni hali ambayo mataifa mengi duniani hukumbana nayo, na mara nyingi matatizo hayo yakitokea huwa hayarudi nyuma kirahisi. Ni wajibu wetu kuendelea kuiombea nchi yetu amani na kuwaombea askari wetu ulinzi na usalama,” alisema Sheikh Kabeke.
Amewataka Watanzania kuendelea kuwalea vijana katika misingi ya maadili mema, kuachana na chuki na wivu, na kuendelea kumuombea Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuongoza nchi kwa amani na umoja.
“Tumuunge mkono Rais wetu. Nani asiyemtaka wakati alipata zaidi ya asilimia 97 ya kura? Tuendelee kumuombea aendelee kuiongoza nchi katika amani na umoja,” aliongeza Sheikh Kabeke.
Kwa upande wake, Sheikh wa Bilal Muslim Kanda ya Ziwa, Hashim Ramadhan, alisema vurugu na taharuki zilizojitokeza ni matokeo ya baadhi ya Watanzania kukosa imani na uvumilivu.
“Badala ya kuishukuru serikali kwa maendeleo mengi yaliyopatikana, baadhi yetu tumekuwa tukihamasishwa na watu wasioitakia mema nchi yetu, hasa wanaoishi nje ya nchi. Wanaeneza chuki na ghasia wakidai nchi ‘inaliwa’, huku wakichochewa na mataifa ya magharibi yanayotuonea wivu kwa kuwa sisi ni kisiwa cha amani,” alisema Sheikh Ramadhan.
Naye Sheikh wa Wilaya ya Misungwi, Hussein Hussein, alisema kabla ya uchaguzi viongozi wa dini walimwomba Mungu kwa ajili ya amani, na kwamba Waislamu wanapaswa kuendelea kuzingatia maelekezo ya Qur’an badala ya kufuata mambo yasiyo na msingi.
“Qur’an inatuelekeza kuwatii viongozi wetu. Oktoba 29, 2025 tulifanya uchaguzi vizuri, lakini saa 10:30 usiku ghafla vurugu zikaanza baada ya vijana kujikusanya na kuharibu mali za watu na miundombinu ya serikali. Dua hii ni ya kumwomba Mungu atusamehe,” alisema Sheikh Hussein.
Aidha, Mjumbe wa Baraza la Masheikh Wilaya ya Nyamagana, Ayub Khatibu, alisema vurugu hizo zilitokana na kukaidi maelekezo ya serikali na viongozi wa dini, akiwataka Watanzania kuendelea kulinda amani na kutii mamlaka.
Sheikh wa Wilaya ya Ilemela, Abdulwarith Jumaa, alisema mkusanyiko huo wa dua ni ishara ya heri na amani, akisisitiza kuwa hakuna jambo lolote linaloweza kufanyika bila utulivu.
“Haya yanayotokea ni kutuonya kuhusu kutoandamana hovyo. Tuna wajibu wa kumuunga mkono Rais Samia. Mungu anatukumbusha kuhusu amani katika Qur’an, Sura ya 15, pale Ibrahim aliposema: ‘Mungu, ujalie mji huu wa Makka uwe wa amani, nilinde mimi na kizazi changu tusije tukaabudu masanamu.” alisema Sheikh Jumaa.
Naye Kadhi wa Wilaya ya Nyamagana, Sheikh Fadhil Ndumiwe, alionya kuwa kutomtii kiongozi ni kujitafutia matatizo, akisema kuwa uasi huleta madhara makubwa kwa mtu na jamii.
“Ukimwasi Mungu unapata dhiki. Ukianzisha vurugu, je, unaweza kuishi kwa amani? Tuhamasishane kuzuia wanaotaka kuvuruga nchi, maana Rais Dk. Samia hajatuamrisha kufanya maovu. Tumuunge mkono kwa nia yake njema ya kuwatumikia Watanzania,” alisema Kadhi Ndumiwe.
Viongozi hao kwa pamoja wametoa wito kwa Watanzania wote kuendelea kuiombea nchi amani, umoja na uongozi wenye hekima, wakisisitiza kuwa amani ni nguzo kuu ya haki na maendeleo ya Taifa.




